Habari Mseto

Mikono ya kijana aliyechomwa sababu ya ugali wa jirani yakatwa

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WANYORO

MADAKTARI katika Hospitali ya Kimisheni ya Consolata, eneo la Nkubu, Meru wamekata mikono ya mvulana aliyechomwa kwa maji moto baada ya kuiba unga wa ugali katika kijiji cha Kargi, Marsabit.

Halkano Sembeni, 11 alikatwa mkono wake wa kulia kuanzia kiwiko kisha vidole vyake vinne vikang’olewa kupitia upasuaji.

Mkurugenzi wa huduma za uuguzi katika hospitali hiyo Julia Muthomi alisema mvulana huyo atalazimika kuwa hospitalini kwa muda mrefu japo hali yake imeanza kuimarika.

“Mvulana anaendelea vizuri na hali yake inaimarika. Atalazimika kuwa hapa kwa muda kwa sababu ana majeraha yatakayochukua muda kupona,” akasema Bi Muthomi.

Mikono ya mvulana huyo ilitiwa ndani ya sufuria yenye maji iliyopashwa moto hadi ikatokota na mwanamume katili. Hii ni baada ya kijana huyo aliyesakamwa na njaa kuingia ndani ya Manyatta na kujipikia ugali alipokuwa akiwalisha mbuzi kando ya Manyatta ya mwanamume huyo.

Naibu Kamishina wa Loyangalani Mutua Njeru alisema polisi katika kituo cha Kargi walimkamata mshukiwa punde tu baada ya unyama huo lakini wakamwaachilia baada ya kukabiliwa na kundi la wanaume wenye bunduki ili kuepuka makabiliano.