Kadinali George Pell apatikana na hatia ya kuwadhulumu wavulana kingono
Na MASHIRIKA
MELBOURNE, AUSTRALIA
MMOJA wa washauri wa karibu zaidi wa Papa Francis ambaye ni mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Kadinali George Pell kutoka Australia amepatikana na hatia ya kuwadhulumu kingono wavulana wawili.
Kisa hiki sasa kimekuwa cha kwanza cha mhubiri wa ngazi ya juu zaidi katika kanisa hilo kuhusishwa na dhuluma za kingono, wakati kanisa hilo linapambana kujikwamua kutokana na tatizo hilo, ambapo wahubiri wake wengi wamelaumiwa.
Mahakama ya Australia ilimpata Kadinali Pell na hatia ya kuwadhulumu kingono wavulana hao, katika mashtaka ya kutenda vitendo vya aibu dhidi ya watoto hao, katika kanisa la St Patricks Cathedral mjini Melbourne, miaka ya tisini.
Kadinali Pell, 77, alipatikana na makosa ya kuwalazimisha wavulana hao ambao walikuwa na umri kati ya miaka 12 na 13 kumfanyia kitendo cha ngono, baada ya misa kukamilika, wakati wa tukio.
Mhubiri huyo ambaye alikuwa huru kwa dhamana, hata hivyo, alikana mashtaka yote aliposhtakiwa na kesi kuamuliwa Septemba 2018, lakini hata baada ya kushtakiwa tena akapatikana na hatia Desemba mwaka uo huo.
Madai yake kuhusika na vitendo vya dhuluma za kingono yameibuka, yakiwa ya kutoka miaka ya ’70.
Mawakili wake walizidi kushikilia kuwa Bw Pell hakufanya kosa lolote, huku makao makuu ya kanisa hilo Vatican yakisalia kimya kuhusiana na kesi hiyo.
Kikao cha kusikizwa kwa kesi hiyo kabla ya kuhukumiwa kitafanyika leo Jumatano ambapo Pell anatarajiwa kutupwa rumande.
Pell amekuwa mmoja wa wandani wakubwa zaidi wa Papa Francis, tangu alipoteuliwa kuwa msimamizi wa Fedha katika kanisa hilo Vatican, mnamo 2014.