Habari MsetoSiasa

Mswada wa Jinsia wafeli mara ya nne mfululizo

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumatano walikaidi vinara wa vyama vyao na kuangusha Mswada wa Jinsia kwa mara ya nne mfululizo.

Kufeli kwa mswada huu kunaashiria kuwa wabunge, hususan wanaume, wamekaidi wito vinara wa vyama vyao, Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto, Raila Odinga wa ODM na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambao walikuwa wamewahimiza kuupigia kura.

Punde baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi kutangaza kuwa mswada huo umeanguka, wabunge wanawake waliapa kutatiza shughuli za serikali bungeni.

Walisema kuanzia sasa hawataunga mkono miswada ya serikali, bajeti ya ziada na marekebisho ya katiba ikiwa malengo ya mswada wa jinsia hayatekelezwa.

Viongozi hao, ambao walionekana wenye hasira, pia walipendekeza bunge livunjiliwe mbali na uchaguzi mpya uitishwe.

“Sasa ni wazi kutojitolea kwa uongozi wa bunge na serikali ndiko kumechangia kufeli kwa mswada huu, ambao unapania kufanikisha azma ya kuhakikisha uwakilishi wa wanawake unaimarishwa bungeni,” akasema Mbunge wa Kandara, Esther Wahome.

Naye mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge Wanawake (KEWOPA), Bi Wangui Ngirici akaongeza: “Kuna unafiki mwingi kwa upande wa uongozi wa bunge na serikali kuhusu masuala ya wanawake. Duale hakuendesha ushawishi wa kutosha, sawa na serikali ambayo haikuonyesha kujitolea kwake kuona kuwa mswada huu umefaulu.”

“Kwa hivyo, tunatangaza kwamba hatutaunga mkono miswada ya serikali, kura ya maamuzi na hata bajeti ya ziada, ikiwa malengo ya mswada huu hayatatekelezwa,” Bi Ngirici, ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga akasema.

Alisema endapo serikali ingetaka mswada huo kupita, ingetumia ushawishi wake kufikia hilo ilivyoshinikiza kupitishwa kwa mswada wa VAT mwaka jana.

Mswada huo wa jinsia ulifeli baada kukosekana kwa idadi ya wabunge 233 waliohitajika kuupitisha. Kulikuwepo na wabunge 174 pekee bungeni saa tisa alasiri, ndiposa Spika Muturi akaamuru kwamba mswada huo usipigiwe kura.

Upigaji kura kwa mswada huo uliahirishwa mnamo Novemba mwaka jana katika mazingira sawa ya kutowepo kwa idadi tosha ya wabunge.