• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Gor pazuri ligini baada ya kuliza miamba Tusker

Gor pazuri ligini baada ya kuliza miamba Tusker

Na WAANDISHI WETU

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia walipaa hadi nafasi ya pili jedwalini baada ya kuwachabanga Tusker FC bao 1-0 Jumatano uwanjani Kenyatta, Machakos.

Bao la pekee na la ushindi kwa Gor Mahia lilijazwa kimiani na fowadi Nicholas Kipkurui aliyeshirikiana vyema na Jacques Tuyisenge mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Tuyisenge aliondolewa ugani katika dakika ya 84 na nafasi yake kutwaliwa na mvamizi Dennis Oliech aliyepoteza nafasi mbili za wazi.

Iliwalazimu Gor Mahia ambao ni wafalme mara 17 wa KPL kucheza zaidi ya dakika 60 za mchuano huo wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya kipa Boniface Oluoch kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 23.

Ingawa Tusker walipachika wavuni mabao mawili, jitihada zao zilifutiliwa mbali na refa kwa kuwa wafungaji walikuwa wameotea.

Tukio hilo lilichangia ufufuo mkubwa wa Tusker walioonekana kuwazidi wenyeji wao katika kila idara mwishoni mwa kipindi cha pili.

Shafik Batambuze (kushoto) wa Gor Mahia awania mpira dhidi ya Kevin Omondi wa Tusker Februari 27, 2019, timu hizi mbili zilipomenyana katika uwanja wa Machakos na Gor kushinda 1-0. Picha/ Sila Kiplagat

Awali katika dakika ya saba, nusura mvamizi Timothy Otieno awaweke Tusker uongozini baada ya kushirikiana vilivyo na David Juma aliyemegewa pasi na John Kamau.

Chini ya kocha Robert Matano, Tusker ambao ni washindi mara 11 wa taji la KPL wanasalia katika nafasi ya sita jedwalini kwa alama 22 sawa na Kariobangi Sharks ambao wanafunga mduara wa saba-bora.

Kwa upande wao, Gor Mahia waliwaruka mabingwa wa 2008, Mathare United ambao kwa sasa wanashikilia wanasalia katika nafasi ya tatu kwa alama 29.

Vijana hao wa kocha Francis Kimanzi wana uchache wa mabao matano ili kuwafikia Gor Mahia ambao wamejizolea magoli 22 na kufungwa manane pekee kutokana na mechi 14 zilizopita.

Nafuu zaidi kwa kikosi hicho cha kocha Hassan Oktay ni kwamba Mathare Utd ambao kwa sasa wanausoma mgongo wao kwa karibu sana, wamesakata mchuano mmoja zaidi, sawa na Sofapaka ambao wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 24.

Gor Mahia walishuka dimbani wakitawaliwa na kiu ya kuendeleza ubabe wao ligini na kuweka hai matumaini ya kutetea kwa mafanikio ufalme wa taji hilo.

Aidha, walikuwa na motisha tele baada ya kupepeta NA Hussein Dey ya Algeria 2-0 katika mchuano wa Kundi D wa kuwania Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF) wikendi jana.

Tusker kwa upande wao walipania kujinyanyua baada ya kuduwazwa na Kakamega Homeboyz kwa kichapo cha 1-0 katika mchuano uliowakutanisha uwanjani Ruaraka wiki jana.

Maandalizi

Tusker kwa sasa wanatarajiwa kuanza maandalizi kwa minajili ya mechi dhidi ya Nzoia Sugar mjini Bungoma kabla ya kushuka dimbani kupimana ubabe na AFC Leopards, Ulinzi Stars na Sharks kwa usanjari huo.

Gor kwa upande wao wana mtihani mgumu zaidi dhidi ya Hussein Dey katika marudiano yatakayowakutanisha nchini Algeria mnamo Machi 3. Baadaye, watavaana na Ulinzi Stars na Homeboyz ligini kabla ya kuwaendea Zamalek SC ya Misri katika mkondo wa pili wa CAF.

Kwingineko, kocha Casa Mbungo wa AFC Leopards amewataka wachezaji wake kujinyanyua mkiani mwa jedwali au la wakabiliwe na shoka litakalowashusha ngazi mwisho wa msimu huu.

Leopards ambao ni mabingwa mara 13 wa KPL walizamishwa kabisa mwishoni mwa wiki jana baada ya kupepetwa 2-0 na Mathare Utd. Ni matokeo ambayo yaliwaweka vijana hao mkiani mwa jedwali kwa alama 10, moja nyuma ya Vihiga United.

Kufikia sasa, Leopards wamesajili ushindi mara mbili pekee, kuambulia sare mara nne na kupoteza mechi nane kati ya 14 za ufunguzi wa msimu huu.

You can share this post!

Jeraha la Fernandinho latia Manchester City pabaya

Prisons yampa Agala utepe tayari kwa CAVB

adminleo