• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Gor kuelekea Misri baada ya mechi ya CAF nchini Algeria

Gor kuelekea Misri baada ya mechi ya CAF nchini Algeria

Na CECIL ODONGO

IMEBAINIKA kwamba Mabingwa mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) Gor Mahia watasalia Kaskazini mwa Afrika kwa wiki moja baada ya kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Hussein Dey ya Algeria Jumapili hii kwenye kipute cha Kombe la Mashirikisho Barani Afrika(CAF).

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa K’Ogalo Omondi Aduda, timu hiyo itaelekea Misri Jumatatu ijayo ili kujifua kwa mechi ya CAF dhidi ya Zamalek itakayosakatwa Machi 9 jijini Cairo, Misri

Gor Mahia waliwakung’uta Zamalek 4-2 katika mkondo wa kwanza wa kipute hicho ulioandaliwa jijini Nairobi.

“Utaratibu wote unaohusisha kusafiri kwetu unaendeshwa na balozi wa Kenya nchini Misri na tumeelezwa kila kitu ki tayari. Baada ya kuchuana na Hussein Dey, tutaelekea Misri ambako tutajifua hadi tuwajibikie mchuano wetu dhidi ya Zamalek Jumamosi ijayo,” akasema Aduda wakati wa mahojiano na dawati la michezo la Taifa Leo Dijitali.

Shafik Batambuze wa Gor Mahia. Picha/ Maktaba

Kikosi cha wachezaji 20 wa Gor Mahia na maafisa wa benchi ya kiufundi, kiliondoka nchini leo ili kuelekea Algeria. Hii ni baada ya serikali kupitia Wizara ya Michezo kuwapokeza wachezaji wote tiketi za usafiri.

“Wizara ya Michezo imetoa tiketi 20 kwa wachezaji, hata hivyo ujumbe wa watu saba unaojumuisha benchi ya kiufundi tiketi zao zitagharimiwa na klabu. Kwa niaba ya uongozi, ningependa kuishukuru sana serikali kwa kutufaa, nawahakikishia tuwakilisha nchi vizuri,” akaendelea Aduda.

Vitisho

Afisa huyo pia alisema hawatayumbishwa na vitisho vya wenyeji wao vya kuwapa mapokezi mabaya na kulitaka Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) kuchukulia Hussein Dey hatua kali za kinidhamu iwapo watatekeleza vitisho hivyo.

“Ninaomba CAF kufuatilia mechi hii kwa makini kwa sababu wenyeji wetu wamenukuliwa wakitisha kufanya kila aina ya hujuma ili kutwaa ushindi. Tulidhulumiwa Angola, Cameroon na Nigeria katika mechi zetu za awali za CAF na hakuna adhabu iliyotolewa kwa klabu husika,” akaongeza.

Gor Mahia wanaongoza kundi D kwa alama sita, alama mbili mbele ya Hussein Dey na Petro Atletico ya Angola walio na alama nne kila moja kisha Zamalek mkiani kwa alama mbili.

You can share this post!

Ufisadi: Raila atofautiana vikali na kauli ya Waititu

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Usihuzunike! Subira wakati wa...

adminleo