Habari Mseto

Wazazi wabaini mbinu ya kukabili mimba za mapema

March 1st, 2019 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WAZAZI wamevumbua mbinu ya kukabiliana na mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi wa shule za Msingi na Upili nchini.

Kulingana na Wizara ya Elimu, kaunti saba nchini ambazo ziliathirika zaidi kutokana na janga hilo ni; Narok, Kilifi, Meru, Bungoma, Busia, Migori, Nairobi na Homa Bay.

Kupitia muungano wa kitaifa wa wazazi nchini, wazazi sasa wanataka wanafunzi wa kiume wanaowatunga wenzao wa kike mimba wachukue jukumu la uzazi.

Mkurugenzi wa Hazina ya Mafunzo ya Matibabu nchini Monica Ogutu akizungumzia suala la afya ya uzazi katika hafla ya awali mjini Kisumu. Wazazi wa Pwani wanataka wanafunzi wa kiume wanaotunga wenzao wa kike mimba wahusishwe kwenye malezi. Picha/ Tonny Omondi

Pia wazazi wanataka vyombo vya serikali kuanza kuwasaka waliowapa wanafunzi mimba na kuwakamata na kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.

“Huwa ninasikitika sana kuona wasichana wakiacha shule sababu ya kutungwa mimba ilhali waliowatunga mimba wanaendelea na maisha yao kana kwanza hapajaharibika jambo,” alisema naibu mwenyekiti wa muungano huo Bi Sarah Kithinji.

Sheria iko wazi

Akiongea kwenye mahojiano ya Elimu katika runinga moja nchini, Bi Kithinji alisema wasichana wanaopewa mimba wakiwa shule ya msingi na upili, wanapaswa kuwataja washukiwa.

Alisema sheria ni wazi kuhusu kushiriki ngono na watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

“Kama aliyekutunga mimba ni mwanafunzi, basi anafaa achukue jukumu lake la kuwa mzazi hususan baba. Msichana akitungwa mimba, ni wazazi wake ambao wanateseka ilhali wazazi wa aliyetunga mimba wakiendelea na maisha yao,” alisema.

Aliwaambia wazazi wa watoto wa kiume katika vyuo vikuu kwamba huenda kuwa wana wajukuu.

“Kama una mtoto wa kiume shule ya Upili au Chuo Kikuu kuna uwezekano kwamba una mjukuu na huna habari,” alisisitiza. Bi Kithinji alisema watoto wa kike wanaopewa mimba huwa ‘wanasulubiwa’.

“Hakuna mazungumzo kuhusu nani aliyemtunga mimba. Wazazi wa mtoto wa kike wanahukumiwa,” alisema.

Bi Kithinji alisema mwanamume anayemtunga mimba anafaa kuandamana na msichana hadi kliniki zake na anapojifungua.

“Kama ni mwanafunzi anafaa awe na sare yake, aandamane na msichana aliyemtunga mimba waende kliniki wote wakiwa na sare za shule anapojifungua awe hapo ndani aone jukumu la kuwa baba au mzazi hapo ndipo wataapoacha kutunga mimba watoto,” alisema Bi Kithinji.

Aliwasihi walimu kuwaruhusu wanafunzi wa kiume waliowatunga wenzao wa kike mimba ruhusa ya kwenda kliniki.

“Kama alitunga mimba aandamane na huyo msichana hadi anapojifungua aone kuwa na mtoto inamaanisha kazi ngumu,” aliongeza.