Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii katika Kiswahili

March 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KING’EI (2010), anasema kwamba kwanza, lugha ni zao la jamii na ni kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika.

Pili, anasema lugha hutumiwa na jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana.Hivyo isimu jamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha.

Uhusiano baina ya lugha na jamii

  1. Lugha ni zao la jamii

Ni sehemu ya jamii kwa kuwa ni sehemu ya utamaduni wa jamii husika. Lugha ni njia inayotumiwa na wanajamii ili kueleza na kusambaza utamaduni wake.

  1. Kwa mujibu wa wanaisimu Sapir na Whorf, lugha huathiri sana na kudhibiti jinsi wazungumzaji na watumiaji wa lugha wa jamii fulani wanavyoufasili ulimwengu wao. Kulingana na wanaisimu hawa muundo wa maana katika lugha ndiyo msingi wa mawazo au utaratibu wa fikra.

Isitoshe, mwanadamu hawezi kufikiri kamwe bila kutumia lugha. Jambo hili linamaanisha kuwa kwa vile mawazo na fikra za mwanadamu vinaukiliwa na lugha basi inawezekana kudhibiti fikra za wanajamii kwa kuidhibiti lugha yao.

Katika muktadha wa nchi nyingi za Kiafrika, hili limethibitika kwa mfano idadi kubwa ya Waafrika wanahusisha maarifa au ustaarabu na lugha ya Kiingereza. Hii inatokana na kasumba potovu iliyoenezwa na wakoloni kwamba lugha ya Kiingereza ni lugha yenye hadhi huku wakidunisha lugha za Kiafrika.

Hivyo, uwezo wao wa kudhibiti matumizi ya lugha kwa kututoa katika matumizi ya lugha mame umefanikisha kuelekeza fikra za wanajamii hawa kwenye mawazo kwamba taaluma na usomi ni kujua Kiingereza.

  1. Kwa mujibu wa King’ei (2010), lugha hurejelea mazingira ya jamii husika, na ndiyo maana watu wenye lugha sawa na wanaoishi katika mazingira tofauti wanaweza kuwa na mtazamo tofauti wa kimaisha na ufasili wao wa ulimwengu.
  2. Kwa kutumia nadharia ya ukiliaji wa kiisimu (Linguistic Determinism) lugha ndiyo inayoongoza mawazo ya watu na huathiri hata maana ambazo watu wanazitoa kuelezea dhana na mitazamo fulani katika lugha zao.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Ipara, I. O., Maina, G. (2008). Fani ya Isimujamii kwa Shule za Sekondari. Nairobi: Oxford University Press (OUP).

King’ei, K., (2010). Misingi ya Isimujamii: Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI). Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar             es Salaam.

Msanjila, Y.P. na wenzake (2010). Isimujamii: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguizi wa Kiswahili (TUKI),               Chuo Kikuu cha Dar es Salaam