• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
USHAIRI WENU JUMAMOSI, MACHI 2, 2019

USHAIRI WENU JUMAMOSI, MACHI 2, 2019

Na MKUSANYAJI WA MASHAIRI

HAYA ni mashairi ambayo yamechapishwa kwenye gazeti la Taifa Leo toleo la Jumamosi, Machi 2, 2019.

 

MWALIMU KAMA MWALIMU

Mwalimu kweli mwalimu, nampongeza mwalimu,
Yeye ni mtu muhimu, mwalimu tumuheshimu,
Ana mengi majukumu, nawajuvya mfahamu,
Hakuna kama mwalimu, sifaze ni nzima chungu.

Hufunza mwenendo mwema, wanafunzi darasani,
Wote wawe na heshima, si Halima si Joani,
Jambo hilo ni adhama, wawe wema maishani,
Hakuna kama mwalimu, sifaze ni nzima chungu.

Hebu tazama rubani, kisha hakimu kortini,
Pia nahodha melini, walifunzwa darasani,
Apewe zawadi gani, huyu mwalimu jamani?
Hakuna kama mwalimu, sifaze ni nzima chungu.

Yeye huwa ni mlezi, kwa walio chekechea,
Huwapa mema malezi, mwalimu amebobea,
Hilo nimelimaizi, huwa yeye awalea,
Hakuna kama mwalimu, sifaze ni nzima chungu.

EBBY SOGONI
‘Nyota ya Amani’
Bungoma

 

KIPUSA NIPOZE NAFSI

Nikubali niwe wako, mrembo mimi nipende,
Nitie rohoni mwako, penzi ja wingu litande,
Nikawe rijali wako, mapenzi kwayo tugande,
Itulize yangu nafsi, kipusa mimi nipende.

Taanusi umbo lako, meshawishi nikupende,
Yavutia sura yako, ngoziyo maji ya kunde,
Lipo tisti ziwa lako, hamna katu upinde,
Itulize yangu nafsi, kipusa mimi nipende.

Sing’oki nazama kwako, moyo naupiga konde,
Nangoja hukumu yako, ghulamu nipo rumande,
Naifuga roho yako, ninawe kila upande,
Itulize yangu nafsi, kipusa mimi nipende.

Msimamo huo wako, ulegeze kwetu twende,
Nilifute chozi lako, kila siku nikulinde,
Huwe wangu niwe wako, maisha raha tuponde,
Itulize yangu nafsi, kipusa mimi nipende.

FELIX GATUMO
‘Malenga Mtamu’
Chuo Kikuu cha Maseno

 

LAANA TAMU

Limefika kileleni, kusheheni kwa haraka,
Janga hili si kubuni, dada zetu wateseka,
Wazee wetu wahuni, na tabia za kubaka,
Kubaka laana tamu, ukatili na unyama.

Mtoto umemzaa, wewe unamnajisi,
Kwa sababu ya tamaa, kutenda ya ibilisi,
Umewadia wasaa, kukomesha mambo hasi,
Kubaka laana tamu, ukatili na unyama.

Ni ajabu ya nguruwe, kummeza mwana wake,
Vipi mzazi mwenyewe, kumla mwanawe?
Umejilaani wewe, heshimu mwana wa kike,
Kubaka laana tamu, ukatili na unyama.

Wanaume nawambiya, mmeikosa nidhamu,
Zote tuavisikiya, vitendo vya kudhalimu,
Aibu mwajipatiya, na akili ni timamu,
Kubaka laana tamu, ukatili na unyama.

FRED OSANDO
‘Mwana wa Isabellah’
Chuo cha Kaimosi

 

TUIGE WATANGULIZI

Washairi tusomeni, tusitunge longo longo,
Makitaba tuendeni, twachetunga tongo tongo,
Na lakabu sijipani, hali hatunao mwengo,
Washairi wa kileo, tuigeni wa zamani.

Twabambanya tu mizani, vina kuvilazimisha,
Utamu haumo ndani, mwa shairi ni maghusha,
Maudhui shairini, hayamo lasikitisha,
Washairi wa kileo, tuigeni wa zamani.

Twafukuza jenga jina, kijinadi makundini,
Maustadhi wa vina, viendavyo ubogoni,
Nasaha leo hatuna, hata tungo si ughuni,
Washairi wa kileo, tuigeni wa zamani.

Malenga ni jina gani, alitwaa kila mtu!
Malenga wa toka lini, na tungoze ni mabutu!
Hu ujuba tuwateni, dhwabiya za makurutu,
Washairi wa kileo, tuigeni wa zamani.

RAMADHAN ABDALLAH SAVONGE
‘Malenga wa Nchi Kavu’
Malalani, Mutitu

 

MAGAIDI HAYAWANI

Nchi imo mashakani, wananchi tu kizani,
Chombo kipo hatarani, kuzamia baharani,
Twasonga kishanishani, lipotoka twarudini,
Magaidi hayawani, mshindwe twawalaani.

Ukienda mabadini, kwa utele washeheni,
Misikiti hekaluni, pia mule kanisani,
Kwa kondoo taficheni, kiwa mbwa wa mwituni,
Magaidi hayawani, mshindwe twawalaani.

Nenda pia mashuleni, magaidi mefikeni,
Nafasi wamejipeni, sekondari na vyuoni,
Wajisifu mesomeni, vyeti ghushi kishikeni,
Magaidi hayawani, mshindwe twawalaani.

Nenda pia makazini, magaidi mefikeni,
Ukipiga darubini, meusi tayapateni,
Kazi watawapeeni, kwavyo vyeti vya kubuni,
Magaidi hayawani, mshindwe twawalaani.

SHUARA MAXYWELLI
‘Malenga Mbichi’
Chuo Kikuu cha Moi

 


UONGOZI SI PAPARA

Uongozi ni heshima, jitu kuutekeleza,
Kuwa na utu uzima, watu kutowapuuza,
Kujitoa kwa ujima, umoja kuendeleza,
Lakini sio papara, kutaka kuogopewa.

Uongozi ni hekima, kuchelea kuhukumu,
Kuwaza kabla kusema, kuvumilia na ghamu,
Kuufungua mtima, kupenda wote dawamu,
Lakini sio papara, kutaka kuogopewa.

Uongozi si dhuluma, maamuma kuwatesa,
Kuwafanya kuangema, na nyoyoni kuwachusa,
Aamuapo Karima, kitakuja chako kisa,
Lakini sio papara, kuatka kuogopewa.

Miye Mwari ninasema, wosia wangu babu,
Kwamba uongozi mwema, ni utu pia adabu,
Ni kujikinga na shutma, na kwa kheri kuatibu,
Lakini sio papara, kutaka kuogopewa.

JUMA MWARI
‘Waridi’
Moi Girls Eldoret

 

NAJITOSA FANINI

Ndugu yangu Ekadeli, nimelitunga shairi,
Nimetunga kwa makali, ila sinao ushari,
Na neno kwenye akili, ninaomba ushauri,
Nami nimeanza kazi, kazi hii ya kutunga.

Usishangae mwenzako, ni nani anayesema,
shaingia kwenye soko, la kutunga na kusoma,
Yanitoka mihemuko, na kutunga sitokoma,
Nami nimeanza kazi, ya kutunga mashairi.

Kiunoni nina kanga, kichwani cheche kalili,
Mashairi nayotunga, ajabu ya kiswahili,
Beti nilizozipanga, zisizokuwa mshikeli,
Nami nimeanza kazi, ya kutunga mashairi.

Balozi nakufuata, ili uweze nifunza,
Wapi nitapokupata, Nairobi ama kwanza,
Sinipe jawabu tata, likuje likaniponza!
Nami nimeanza kazi, ya kutunga mashairi.

CEDRIC OGETO
‘Cedo’
Kitale

 

PENZI LIANZAPO KUFA

Kwanza, mawasiliano, kasi yake hupunguwa,
Hayawi masemezano, ja mwanzo yalivyokuwa,
Hata soga na vigano, hukoma pasi kujuwa,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

Pili, ni mifarakano, hutokea kila mara,
Muda wote mivutano, ambayo haina dira,
Huwa shida mapatano, hii ni mbaya bishara,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

Tatu jambo la dharau, huanza kuonekana,
Kuonana mabahau, kwenye vitu viso ma’na,
Wakati kumbe walau, mwaweza eleweshana,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

Nne kuaminiana, huwa ni kitendawili,
Kwake bibi pia bwana, jambo hili linajili,
Mitego hutegeana, ashikwe mwizi kamili,
Penzi lianzapo kufa, dalili zake ni hizi.

MFAUME HAMISI
‘Mshairi Machinga’
Dar es Salaam, Tanzania

 

NINGEPENDA!

Pulika changu kipenzi, nikweleze ya moyoni,
Mambo haya nayaenzi, kuyatenda natamani,
Tuyafanye kwa vitenzi, wala sio midomoni,
Nisikize kwa makini, ninapokusimulia.

Ningependa tuyasome, mabuku yetu kwa nguvu,
Kwa taa au umeme, usitwingie uvivu,
Mbeleni tuje simama, tazetu ziwe angavu,
Nisikize kwa makini, ninapokusimulia.

Ningependa hisabati, unifunze niijue,
Ikitupata bahati, magari tuyanunue,
Nikupe msamiati, wadaku uwazuzue,
Nisikize kwa makini, ninapokusimulia.

Ningependa mashairi, nikufunze uyatunge,
Japo mie si mahiri, beti zote uzipange,
Ukitaka tafsiri, niambie sijifunge,
Nisikize kwa makini, ninapokusimulia.

GILBERT KINARA
Keumbu, Kisii

 

ULAZWE PEMA MWATHA

Sote wanaharakati, twamomboleza shujaa,
Hakika lijizatiti, kuwaokoa jamaa,
Mjasiri kwa umati, maovu liyakataa,
Ulazwe pema pa wema, Bi Caroline Mwatha.

Vijana alinusuru, aliwapa mashauri,
Uwizi wa misururu, kabisa watahadhari,
Dandora likuwa nuru, lino mjue dhahiri,
Ulazwe pema pa wema, Bi Caroline Mwatha.

Alitaka haki wazi, binadamu kupatiwa,
Ni shupavu kiongozi, tunapasa kutambuwa,
Malenga Mpelelezi, natowa yangu makiwa,
Ulazwe pema pa wema, Bi Caroline Mwatha.

Marafiki familia, twamombea kwa Rahimu,
Jambo moja twalilia, haki usawa udumu,
Yote tunamuachia, Maulana kuhukumu,
Ulazwe pema pa wema, Bi Caroline Mwatha.

MUKOYA AYWAH
‘Malenga Mpelelezi’
Lang’ata, Nairobi

You can share this post!

USHAIRI WENU: Kazi nitazochapa

SHANGAZI AKUJIBU: Mwanamume nimpendaye amezingirwa na...

adminleo