Habari

Ufisadi: Nani msema kweli?

March 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

UCHUNGUZI kuhusu sakata ya ujenzi wa mabwawa mawili katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet umeibua joto huku viongozi, maafisa wa serikali wakitofautiana na ripoti ya upelelezi na kurushiana lawama.

Huku lawama hizo zikiendelea, Wakenya wanajiuliza nani anayesema ukweli kati ya wapelelezi wanaosisitiza kuwa serikali ilipoteza pesa na wanaodai kwamba hazikupotea.

Viongozi wa kisiasa kutoka eneo hilo wakiongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen wanakanusha ripoti ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kwamba serikali ilipoteza Sh21 bilioni kwenye sakata ya ujenzi wa bwawa la Kamwerer na Arror.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti. Picha/ Maktaba

Kulingana na Dkt Ruto, ripoti ya DCI ni uongo mtupu kwa kuwa ni Sh7 bilioni pekee zilizolipwa kampuni iliyopewa kandarasi ya kujenga mabwawa hayo mawili kwa jumla ya Sh63 bilioni.

“Ni uongo mtupu. Tumeweka mikakati ya kulinda pesa za umma,” Dkt Ruto alisema.

Akizungumza mnamo Alhamisi katika Mahakama ya Juu mbele ya Rais Uhuru Kenyatta na Jaji Mkuu David Maraga, Dkt Ruto alisisitiza kuwa hakuna pesa zilizopotea kwa sababu mkandarasi alikuwa ameweka dhamana katika benki.

Saa chache baada ya Bw Ruto kutoa kauli hiyo, Bw Murkomen alitoa taarifa katika seneti akilaumu DCI kwa kuhujumu miradi inayolenga kunufaisha wakazi wa Elgeyo Marakwet.

Bw Murkomen alisema ujenzi wa mabwawa hayo umeingizwa siasa na Bw Kinoti anatumiwa kummaliza Naibu Rais William Ruto kisiasa.

“Sifurahishwi na jinsi uchunguzi kuhusu sakata za ufisadi unavyoendeshwa. Kwangu mimi, Bw Kinoti anatumiwa na watu kummaliza kisiasa Bw Ruto,” alidai akihojiwa na runinga ya Citizen mnamo Alhamisi usiku.

Kulingana na Mamlaka ya Ustawi wa Bonde la Kerio (KVDA) Sh4.2 bilioni zililipwa kwa ujenzi wa bwawa la Arror mnamo Desemba 2017 na Sh3.4 zililipwa kwa ujenzi wa bwawa la Kimwarer mnamo Novemba 2018.

Wapelelezi wanataka kujua kwa nini pesa hizo zililipwa kwa kampuni iliyofilisika CMC Di Ravenna bila kubaini ikiwa ilikuwa na uwezo wa kujenga mabwawa hayo. Wanasema pesa hizo zililipwa hata kabla ya wakazi wanaoishi katika maeneo ambayo mabwawa yalinuiwa kujengwa kulipwa fidia na kuhusishwa katika mipango ya ujenzi wa mabwawa yenyewe.

Bw Kinoti anasema baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini waliowezesha pesa hizo kulipwa, walipata hongo kutoka kwa kampuni hiyo.

Lakini kulingana na KVDA na Wizara ya Fedha ambayo waziri wake Henry Rotich alihojiwa na wapelelezi, hapakuwa na makosa katika kulipa pesa hizo ikiwa sheria zilifuatwa.

“Pesa zinazolipwa mkandarasi kabla ya kuanza kazi huwa ni mkopo unaolipwa wakati wa malipo baada ya kazi. Malipo haya huwa katika kandarasi zote za aina hii,” ilisema taarifa ya KVDA.

Taarifa ya wizara inasema kwamba kampuni na mashirika mengine yaliyohusika katika kandarasi hiyo kama maajenti pia walilipwa mabilioni ya pesa.

Inataja ada hizo kama za bima zilizolipwa kampuni ya Space Insurance Premium Sh6.1 bilioni kwa bwawa la Arror na Sh5 bilioni kwa bwawa la Kamwerer.

Kulingana na Wizara ya Fedha, Sh3.5 milioni zililipwa kama ada za wakala miongoni mwa ada nyingine za kima cha Sh905 milioni.

Baadhi ya ada zilizolipwa mawakala, haziwezi kurudishwa kwa sababu ni masharti yanayotangulia kandarasi.

Wizara ya Fedha, kwenye taarifa ilitofautiana na Bw Murkomen kwa kusema kwamba baada ya kupokea malipo, kampuni hiyo ilipaswa kuanza kazi chini ya usimamizi wa KVDA na wizara husika mara moja.

‘Si mara ya kwanza’

Kwenye mahojiano yake na runinga ya Citizen, Bw Murkomen alisema haikuwa mara ya kwanza mradi kuchelewa kuanza nchini.

Wizara hiyo ilisema iwapo uchunguzi utabaini kuwa masharti ya kandarasi yalikiukwa, waliohusika wanafaa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kauli hii ni tofauti na Bw Murkomen na Bw Ruto ambao wanasisitiza kuwa hapakuwa na makosa yoyote.