Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana ya lugha na utamaduni ikiwemo uhusiano uliopo

March 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KWA kuzingatia Nadharia ya Sapir na Whorf, tunapata kwamba kuna uhusiano wa lugha na utamaduni katika jamii.

Nadharia hii inasema kwamba lugha hutawala namna wazungumzaji wake wanavyoiona dunia.

Kwa kuchunguza baadhi ya misamiati ya wanalugha fulani, utagundua yapo maneno pekee yanayowakilisha yale wanayoona mbele ya macho yao au mazingira yao tu na kutokuwepo kwa neno kunamaanisha kwamba jambo hilo halipo ‘machoni’ pao.

Sawa na kusema kuwa ‘lisilokuwepo machoni na moyoni halipo’.

Lugha ya mtu hutawala mawazo yake.

Dhana tulizonazo huunda kile tunachokiona, kinachotuzingira na kinachotuhusu.

Lugha ni mfumo wa dhana, ni mhimili wa jinsi tunavyoiona dunia yetu ya kila siku.

Nida (1986), anasema kuwa, lugha ni kielelezo cha utamaduni wa wazungumzaji wake na sio mhimili wa mtazamo wao. Lugha hufuata jamii na wala si kuiongoza jamii hiyo.

Utamaduni

Dhana ya utamaduni inarejelea jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake.

Utamaduni unajumuisha vipengele vifuatavyo:

  1. Ujuzi
  2. Imani au itikadi
  3. Sanaa
  4. Maadili
  5. Sheria au kanuni
  6. Desturi na vinginevyo

Hivi ni vipengele ambavyo mtu anarithishwa na kujitwalia kama mwanajamii.

Utamaduni pia unaweza kuangaziwa kama mojawapo ya sifa mahususi ya binadamu inayomtofautisha na wanyama.

Aidha, utamaduni ni suala la msingi katika anthropolojia linalohusisha yale yote yanayopokezwa katika jamii fulani, mathalani lugha inayounganisha watu wanaohusika nao, fasihi mafungamano ndoa, ibada, michezo, sayansi na teknolojia.

Ustaarabu

Dhana ya ustaarabu inarejelea utamaduni ulioendelea.

Ni muhimu kufahamu kwamba kila utamaduni unabadilikabadilika mfululizo ndani ya watu husika ambapo baadhi wanachangia na kuunga mkono mabadiliko, huku wengine wakiyakataa na kuyapinga.

Mabadiliko katika utamaduni wa jamii yanachochewa na ujuzi mpya na teknolojia, pamoja na mahitaji ya uchumi.

Ninaandaa matini ya kuchambua kwa kina mada kuhusu historia na maendeleo ya utamaduni katika Kiswahili.

Vilevile, nitaangazia vipindi mbalimbali vya kihistoria na jinsi wataalamu husika walivyochangia katika kuendeleza dhana ya utamaduni katika jamii.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

 

Marejeo

Masebo, J. A., & Nyangwine, A. D. (2002). Nadharia ya Lugha: Kiswahili 1. Dar es Salaam: Afroplus Industries Ltd.

Halliday, M. A. K. (2003). On Language and Linguistics, (Jonathan Webster ed.) ContinuumInternational Publishers.

Masamba, D. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.