Gor Mahia kucheza Jumapili dhidi ya wenyeji Hussein Dey
Na GEOFFREY ANENE
KLABU ya Gor Mahia ilifunga safari Ijumaa jioni kuelekea nchini Algeria kwa mechi muhimu ya marudiano ya Kombe la Mashirikisho la Afrika ya kundi D dhidi ya Hussein Dey.
“Gor Mahia itaelekea Algeria leo (Ijumaa) jioni kushiriki mechi ya Kombe la Mashirikisho la Afrika dhidi ya NA Hussein Dey itakayosakatwa Jumapili, Machi 3. K’Ogalo kisha itapiga kambi mjini Cairo kwa siku sita kabla ya kumenyana na Zamalek mnamo Machi 10,” mabingwa hawa mara 17 wa Kenya walitangaza habari hizi zao za usafiri kupitia mtandao wao wa kijamii wa Twitter, Ijumaa.
Vijana wa kocha Hassan Oktay wanaongoza kundi hili kwa alama sita baada ya kulima Zamalek kutoka Misri 4-2 na Hussein Dey 2-0 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi na kuelemewa 2-1 na Petro de Luanda nchini Angola mwezi Februari.
Gor, ambayo rekodi yake nje ya Kenya ni ya kusikitisha, itajiweka pazuri kuingia robo-fainali ikipata alama ugenini Algeria na hata nchini Misri.
Kwa sasa, Gor inafuatiwa kwa karibu na Petro na Hussein Dey, ambazo zimezoa alama nne kila mmoja kutokana na ushindi mmoja, sare moja na kichapo kimoja, nayo Zamalek inavuta mkia baada ya kupiga sare mbili na kupoteza mchuano mmoja.
Timu zitakazomaliza makundi A, B, C na D katika nafasi mbili za kwanza zitaingia robo-fainali, huku mbili za mwisho zikibanduliwa nje. Mwaka 2018, Gor iliaga mashindano katika awamu hii baada ya kumaliza Kundi D katika nafasi ya tatu nyuma ya USM Alger kutoka Algeria na Rayon Sport ya Rwanda, huku Yanga kutoka Tanzania ikivuta mkia.