• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
Huzuni sokoni baada ya askari rungu 5 kuuawa

Huzuni sokoni baada ya askari rungu 5 kuuawa

Na DERICK LUVEGA

HALI ya huzuni ilitanda katika eneo la Kilingili mpakani mwa kaunti za Vihiga na Kakamega baada ya askari rungu watano kupatikana wameuawa na watu wasiojulikana.

Walinzi hao watano wote wa umri wa zaidi ya miaka 60, wanaaminika kuuawa usiku wa kuamkia Jumapili.

Waathiriwa walikuwa na majeraha kichwani, ishara kwamba waligongwa na vifaa butu.

Familia ya mmoja wa waathiriwa, Bw Thomas Lusioli, 70, ilidai kuwa mwendazake aliwahi kuwaelezea kuwa amekuwa akipokea vitisho kazini.

Binti ya mwendazake, Jane Minao pamoja na kaka zake Stephen Minao na Caleb Minao walisema kuwa baba yao alipokea vitisho Jumanne, siku tano kabla ya kupatikana ameuawa.

Watatu hao, hata hivyo, hawakufichua aliyemtishia baba yao na sababu ya kumfanya kutishiwa.

Mwathiriwa au familia yake hawakuripoti vitisho hivyo kwa polisi.

“Baba yangu alikuwa akifanya kazi ya ulinzi katika soko la Kilingili kwa zaidi ya miaka 10. Jumanne, alitwambia kuwa alitishiwa kazini na akamfahamisha mwajiri wake,” akasema Bi Minao.

“Alipokea vitisho hivyo tena Ijumaa,” akaongezea bila kusema vitisho hivyo vilitoka kwa nani.

Maiti

Maiti ya waathiriwa wanne ilisalia katika eneo la mkasa jana kwa muda mrefu huku maafisa wa usalama wakifanya kikao cha dharura.

Maiti ya waathiriwa hao ilitapakaa katika maeneo mbalimbali ya soko hilo, ishara kwamba wauaji waliwakimbiza kabla ya kuwaua.

Mwathiriwa wa tano, Bw Charles Kalume, 60, alikimbizwa katika hospitali ya Mbale lakini akaaga dunia alipokuwa akiendelea kutibiwa.

Waathiriwa wengine watatu hawakutambuliwa mara moja. Polisi wanashuku kuwa watano hao walishambuliwa na wahalifu waliokuwa na silaha butu.

Walikuwa wakilinda maduka ambayo wahalifu hao walivunja milango na kuingia ndani lakini hawakuiba chochote.

Polisi wanashuku kwamba lengo la wahalifu hao lilikuwa kuua na wala si kuiba.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Vihiga Hassan Barua alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku wakazi wakilaumu polisi kwa kuzembea kazini.

You can share this post!

JAMVI: Kibarua kigumu kwa Ruto kuokoa jahazi la Jubilee...

Wakati wa kuvunja serikali umefika, viongozi Rift Valley...

adminleo