Furaha kijijini aliyefungwa miaka 10 kwa ubakaji akirejea
NA GEORGE MUNENE
VIFIJO na nderemo zilitanda Jumamosi katika kijiji cha Muthani, Kaunti ya Embu, mfungwa aliyekamilisha kifungo cha miaka 10 kwa ubakaji alipoungana na familia yake.
John Mutegi, ambaye alikamilisha kifungo katika gereza la Kamiti jijini Nairobi mwezi mmoja uliopita, alijawa na furaha tele aliporudishwa kijijini mwake na waumini wa Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA) la Cianyi lililoko Kaunti ya Kajiado.
Washirika na wanakijiji walitazama kwa furaha pale babake, Mzee Paul Mugo, aliye na miaka 72, alipomlaki na kumkumbatia mwanawe huku wote wakitiririkwa na machozi ya furaha mbele ya waumini na wanakijiji.
Mzee Mugo, pamoja na mkewe, walitaja kurejea kwa mwanao kama muujiza ambao hawakuutarajia maishani mwao.
“Hatukujua alikoenda mtoto wetu. Tulimtafuta kila pahala bila mafanikio na tukapoteza matumaini ya kuwahi kumwona tena,” akasema mamake, Virginia Wawira.
Makaribisho hayo pia yalivutia naibu chifu wa eneo hilo, Bi Juliet Njuki, ambaye alimhakikishia mfungwa huyo wa zamani kuwa serikali imejitolea kumhakikishia usalama wake usiku na mchana baada ya kubadili mienendo yake.
“Huyu kijana amebadilika na ndiyo sababu nimekuja hapa kumpa makaribisho ya kipekee katika jamii yetu. Yeye sasa ni mmoja wetu,” akasema Bi Njuki.
Alipofika kijijini, Bw Mutegi alilakiwa na wanakijiji waliomkimbilia, kumkumbatia, kumbeba juu juu na kumwimbia nyimbo za furaha.
Wanakijiji hao waliahidi kwamba watasimama na Bw Mutegi na kumpa usaidizi wowote atakaohitaji.
“Tumefurahi sana kuwa wenyeji wamemkubali tena kama mmoja wao,” akasema kiongozi wa kitengo cha waumini wa kuhudumia jamii katika kanisa la Cianyi SDA, Elijah Munayo.
Bw Mutegi alitoroka nyumbani alipoacha masomo akiwa darasa la tatu mnamo 2003 na kuelekea katika kijiji cha Ongata Rongai, alikoajiriwa kuchunga mifugo.
Hata hivyo, alikamatwa na polisi mnamo 2007 kwa kumbaka mjakazi. Mahakama ilimpata na hatia na akahukumiwa miaka 10 gerezani.
Baadhi ya nduguze na dadake hawakuweza kumkumbuka kwa kuwa walikuwa wadogo sana wakati alipotoroka nyumbani.
Bw Mutegi alisimulia umati huo jinsi maisha ya jela yalivyokuwa magumu, na namna nusura apoteze maisha yake wakati mmoja kwa kuugua ugonjwa wa kifua kikuu akitumikia kifungo.
Pia alieleza kuwa kipindi chote akiwa gerezani hakutembelewa na mtu yeyote wa familia yake.