WAKILISHA: Mbona nyota ilizima ghafla?
Na PAULINE ONGAJI
UNAPOKUTANA na Susan Gatwiri, 21, katika mtaa wa Skuta, Kaunti ya Nyeri, akiendelea na kazi yake ya kawaida kama mjakazi ili kukidhi mahitaji yake na jamaa zake, utadhani hana chochote cha kujivunia wakati ana mengi yanayotamanika na wengi.
Gatwiri ni mmojawapo wa chipukizi ambao wamewahi kupeperusha bendera ya Kenya ughaibuni.
Hata hivyo, fahari aliyoiletea nchi hii inadhihirika tu unapopata fursa ya kusafiri hadi nyumbani kwao katika kijiji cha Judeya, eneo la Naro Moru, Kaunti ya Nyeri.
Kando na hati kadha wa kadha zinazoashiria kushiriki kwake katika mashindano mbalimbali, anatoa nishani mbili za dhahabu alizoishindia nchi hii katika Olimpiki za walemavu, mashindano yaliyoandaliwa nchini Amerika mwaka wa 2015.
Alishinda nishani za dhahabu katika mbio za mita 3000 na 5000, na hivyo kuwa mmojawapo ya wanaspoti walioitambulisha Kenya katika mashindano hayo.
Gatwiri aliyezaliwa na matatizo ya kusoma na kuandika, kama watoto wengine walemavu hasa kutoka familia ya kipato kisicho cha kuridhisha vile, hakuwa na matumaini ya kuendelea mbali kimasomo kwani mamake Judith Kiende, hakuwa na uwezo wa kugharimia elimu maalumu, vilevile kushughulikia mahitaji ya nduguze watano.
Ingawa hivyo, kidogo matumaini yalianza kumjia akiwa katika darasa la nne, wakati huo kama mwanafunzi wa shule ya msingi ya Meere huko Naro Moru, ambapo alitambua kipaji chake cha kukimbia.
Penzi lake kwa mchezo huu lilinoga alipozidi kushinda mbio tofauti za mashinani, na katika harakati hizo kupata vyeti na mataji kadha.
Aiwakilisha Kenya
Furaha kuu ilimjia alipofuzu kuiwakilisha Kenya katika michezo ya olimpiki ya walemavu mwaka wa 2015.
“Mwanzoni sikuwa naamini. Nilisadiki nilipojiona nikiwa ndani ya ndege kuelekea nchini Amerika,” aeleza Susan.
Ndoto yake ilitimia kabisa baada ya kushinda nishani mbili za dhahabu na hivyo kuvunja mipaka na hata kujulikana katika mataifa ya ng’ambo.
Fahari zaidi kwake na wenzake walioshiriki kwenye michezo hiyo ilionekana waliporejea nchini na hadithi zao kupamba vichwa vya habari.
“Ilikuwa furaha kuu baada ya kujiona magazetini pamoja na wenzangu tulioshiriki na kushinda katika mashindano hayo,” asema.
Lakini licha ya ufanisi huu uliomfanya hata kutambuliwa katika tuzo za Soya mwaka huo, utambuzi ulioambatana na zawadi ya kitita cha Sh70,000, Gatwiri anaendelea kupambana na ufukara.
Mwanariadha huyu anasema kwamba hakupokea chochote kutokana na ufanisi huu licha ya taarifa za majuma kadha yaliyopita kutoka kwa shirikisho la Olimpiki za Walemavu nchini kwamba alipaswa kupokea Sh200,000 kwa kila nishani ya dhahabu aliyopokea.
Familia yake inalazimika kuendelea kupambana na hali ngumu.
Mamake ambaye anauguza jeraha mkononi baada ya kuanguka miezi kadha iliyopita, anaishi katika nyumba ya matope ya vyumba viwili katika ardhi ya kukodisha.
“Anaishi pamoja na ndugu zangu. Jeraha hili limeathiri jitihada zake za kutafuta riziki ambapo sasa familia yangu yote inanitegemea mimi,” aeleza.
Haya ni baadhi ya matatizo ambayo Gatwiri amekuwa akikumbana nayo na hivyo kumlazimu kutafuta ajira kama mjakazi, kazi ambayo amekuwa akiifanya tangu mwaka 2017.
“Nilipata alama 105 katika mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka wa 2017, alama ambazo hazingeniwezesha kupata nafasi katika shule ya upili, na nilikuwa nadhani kwamba ningepokea pesa hizo ili kupata mafunzo ziada. Lakini niliposubiri bila mafanikio niliamua kufanya kazi hii ambayo inaniwezesha kumsaidia mamangu na mahitaji ya kila siku ikiwa ni pamoja na kumlipia karo dadangu ambaye yuko katika shule ya upili,” aongeza.