Mshindi wa kamari ajutia kuacha kazi kwa dharau
Na Leah Makena
MSAMBWENI, LUNGA LUNGA?
Jamaa wa hapa alijutia hatua yake ya kuacha kazi aliposhinda kitita cha pesa kwenye kamari, biashara aliyofungua ilipofilisika baada ya miezi mitatu.
Yasemekana jamaa aliacha kazi kwa dharau na kujitenga na wenzake akisema alikuwa amevuka daraja na kuwa tajiri.
Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa na kazi ya mshahara mdogo lakini iliyomsaidia kukidhi mahitaji yake na ya familia yake.
Hivi majuzi, kalameni alijitosa kwenye ulingo wa mchezo wa kamari kujaribu bahati yake. Mambo yalimwendea vyema kwani baada ya kujaribu mara kadhaa aliibuka mshindi na akakabidhiwa kitita chake.
Wenzake waliokuwa wamejaribu kamari kwa muda mrefu bila mafanikio walimwambia alikuwa na bahati na kumtaka awaandalie karamu washukuru Mungu pamoja naye.
Hata hivyo jamaa alikataa na hata kuapa kutoripoti kazini na badala yake akafungua kibanda cha kuuza matunda.
Mambo yalikuwa shwari kwa miezi ya kwanza lakini baadaye, biashara ilienda chini kiangazi kilipokumba eneo alilokuwa akitoa matunda na wanunuzi wakapungua pia.
Jamaa aligeukia pesa za biashara na kuanza kuzitumia kwa mahitaji ya kila siku. Haikuchukua muda mrefu kwani alifilisika na akasalia kujutia kuacha kazi yake.
Penyenye zasema kuwa baadhi ya watu walianza kumcheka kwa kushindwa kuendeleza biashara yake licha ya kujigamba hadharani kwamba angekuwa mfanyabiashara wa kutajika baada ya miezi michache.
Minong’ono yasema kwamba jamaa alidai wenzake walimuendea kwa mganga ili kuzuia mafanikio yake hasa alipodinda kuwaandalia karamu na kuwakopesha pesa na kuanza kuwadharau akisema walikuwa masikini.
Hata hivyo, hakuna aliyeweza kuthibitisha madai hayo.