• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Ujenzi wa mabwawa uendelee, utaleta amani – Wabunge

Ujenzi wa mabwawa uendelee, utaleta amani – Wabunge

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa kutoka Kaunti ya Elgeyo Marakwet wamesema kuwa wanaunga mkono uchunguzi unaoendelea kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika mpango wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Wakiwahutubia wanahabari Jumanne, viongozi hao walisema miradi hiyo sharti iruhusiwe kuendelea hadi mwisho kwa sababu itawaletea manufaa makubwa wakazi wa Elgeyo Marakwet na kaunti jirani.

“Miradi hiyo itaziwezesha zaidi ya familia 150,000 kupata maji safi ya matumizi na ya unyunyiziaji ya mashamba ya ukubwa wa ekari 10,000 katika kaunti za Baringo na Elgeyo Marakwet. Itasaidia katika uzalishaji wa megawati 80 za umeme,” akasema mbunge wa Marakwet Magharibi William Kisang’.

Aliandamana na wabunge wenzake; Kangogo Bowen (Marakwet Mashariki), Daniel Rono (Keiyo Kusini) na Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo Jane Chebaibai Kiptoo.

Viongozi hao walisema kuwa manufaa ambayo yataletwa na kufanikishwa kwa miradi hiyo yatachangia kukuza amani kati ya wakazi wa kaunti ya Elgeyo Marakwet kaunti jirani za Baringo na Turkana.

“Kwa muda mrefu eneo kaunti yetu imeathirika na visa vya wizi wa mifugo, ujangili na mapigano ya kikabila. Baada ya ujenzi wa mabwa haya kumalizika tunaamini kuwa shida kama hizo zitakoma,” akasema Bw Bowen.

Bw Rono aliitaka Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kuanza mpango wa kuwalipa ridhaa wakazi ambao ardhi yao ilitwaliwa kwa ujenzi wa mabwawa hayo.

“Tunajua kuwa serikali imetenga Sh650 milioni katika bajeti ya mwaka ujao wa matumizi ya fedha kwa ajili ya ulipaji ridhaa kwa wakazi ambayo ardhi zao zilitwaliwa kutumika kwa miradi hii. Lakini fedha hizo hazitoshi kwa sababu ridhaa kamili inapasa kugharimu Sh6 bilioni,” akasema Bw Rono.

Bi Kiptoo aliuliza ni kwa nini miradi ya ujenzi wa mabwawa hayo mawili ndio inaangaziwa zaidi na kuhusishwa na sakata ilhali kuna zaidi ya miradi 57 ya mabwawa kote nchini.

“Ingawa tunaunga mkono uchunguzi unaoendelea, isiwe kwamba zoezi hilo linalenga kuhamisha mradi huo kwingineko. Katu hatutaruhusu mabwawa hayo kuhamishwa,” akasema Bi Kiptoo.

You can share this post!

Afueni kwa Jumwa

Ujenzi wa mabwawa ya Sh188 bilioni wasitishwa

adminleo