Mgomo wa wafanyakazi watatiza usafiri wa ndege JKIA
Na PETER MBURU
WASAFIRI wa ndege Jumatano waliamkia kuhangaika katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya kuanza kwa mgomo wa Wafanyakazi wa Usafiri wa Angani (Kawu) wakisusia mpango wa kutaka uwanja huo usimamiwe na Kampuni ya Kenya Airways (KQ).
Kumekuwa na vuta nikuvute miongoni mwa washikadau mbalimbali baada ya habari kuibuka kuwa Mamlaka inayomiliki Viwanja vya Ndege (KAA) inapanga kuipokeza kampuni hiyo ya KQ usimamizi wa uwanja wa JKIA.
Wafanyakazi wa uwanja huo kupitia muungano wao wa Kawu wiki iliyopita waliwatahadharisha wasafiri wa ndege kuwa tayari kwani wangeanza mgomo Jumatano, Machi 6, na punde tu ilipofika, wote kwa pamoja walisusia kazi.
Wengi wa wasafiri baada ya kufika katika uwanja huo na kukosa huduma walieleza kuhuzunishwa kwao na hali hiyo kwenye mitandao ya kijamii, kwenye mtandao wa Twitter wakiunda hashtag #JKIA kulalamika namna wamehangaika.
Baadhi yao walisema kuwa walifika eneo hilo takriban saa tisa usiku, japo hakuna kazi yoyote iliyokuwa ikiendelea.
“Mgomo wa KAA umeanza, wasafiri wamezubaa kuanzia saa tisa alfajiri,” ameandika Stanley Mukui.
Wasafiri wengine pia walilalamika kuwa walifaa kuanza safari zao mapema ili wakaunganishe na zingine, lakini mgomo huo ukaathiri mambo.
“Mimi ni miongoni mwa wateja ambao wameachwa bila kuhudumiwa, kila kitu kimezimwa na kuna baridi kali huku nje,” msafiri mwingine akasema.
Lango kuu lafungwa
Hadi asubuhi jua likichomoza, wasafiri bado walikuwa wamepiga kambi nje ya uwanja huo, wakisema kuwa lango kuu lilikuwa limefungwa na kuwa hakuna mfanyakazi aliyekuwa kazini.
Wafanyakazi hao wamepinga kuwa kampuni ya KQ haiwezi kusimamia uwanja huo kwani imekuwa ikiingiza hasara na hivyo itaharibu usimamizi wa uwanja huo.
Viongozi mbalimbali aidha, wakiwemo wabunge na maseneta wamezua pingamizi kuhusu mpango huo, wakisema hawataruhusu hilo kufanyika.