Habari

Mgomo watatiza shughuli JKIA

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

NDEGE ambazo zilikuwa zimepangiwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jumatano zilielekezwa hadi Mombasa na Tanzania kufuatia mgomo wa wafanyakazi ulioanza tangu usiku wa manane.

Mgomo huo ambao uliitishwa na wafanyakazi wanachama wa KAWU umetatiza hali ya kawaida katika uwanja huo wenye utitiri wa shughuli huku maelefu ya abiria wakikosa kusafiri.

Duru ziliambia Taifa Leo Dijitali kwamba wafanyakazi hao waligoma kupinga mpango wa kuwezesha Shirika la Ndege Nchini (KQ) kusimamia shughuli za uwanja wa JKIA, kwa kipindi cha miaka 30.

Wabunge wamepinga mpango huo.

“Tunawashauri abiria wote kuwasiliana na mashirika ya ndege ambayo walipanga kutumia kupata habari kuhusu mipango yao ya safari,” Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege (KAA) ilisema Jumatano asubuhi kwenye taarifa.

Baadhi ya abiria waliweka jumbe za malalamishi katika mitandao ya kijamii huku KAA ikitoa hakikisho kuwa hali ya kawaida itarejea muda si mrefu.

“Nilikuwa nikipanga kusafiri kuelekea Oslo kutoka JKIA Jumatano asubuhi lakini sasa ninaelekea Tanzania ili niweze kupanga upya safari yangu,” Jacob Abere Matlala amesema.

“Huu ni uwanja wa Ndege wa Kimataifa. Tukio hilo linaonyesha picha mbaya zaidi na Viwanja vingine vya ndege nchini Ethiopia, Uganda, na Tanzania vitanufaika. Kile ambacho polisi wanafanya ni kibaya hata zaidi,” akasema mmmoja anayefahamika kama Sam kupitia Twitter.

Polisi na maafisa wa kikosi cha kukabiliana na fujo (GSU) walikabiliana na wafanyakazi hao kwa kuwarushia gesi za kutoa machozi.

Ndani

Katibu Mkuu wa chama cha KAWU Moses Ole Ndiema alikamatwa na polisi kwa kuchochea mgomo huo.

Hali ilikuwa mbaya katika uwanja huo kwani malori ya polisi ya kunyunyiza maji ya kuwasha yalionekana yakiingia humo huku wenye magari ya kibinafsi wakizuiwa kuingia.

Abiria wengi walionekana wakikaa nje ya maeneo ya kuingia na kutoka katika eneo la kupandia ndege.

Baada ya muda Shirika la Ndege Nchini (KQ) lilitoa taarifa likisema kuwa safari za ndege zitacheleweshwa.

“Shirika la Kenya Airways lingependa kuwajulisha wateja wake kwa kutokana na mgomo haramu ulioitishwa na Chama cha Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege (KAWU), shughuli za usafiri za ndege za shirika hilo zitatatizwa,” taarifa ya KQ ilisema.