Chelugui ajitenga na sakata ya uchimbaji mabwawa
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Maji, Simon Chelugui, Jumanne aliwaambia wabunge kwamba mabwawa ya Arror na Kamwerer yanayomulikwa kuhusiana na sakata ya kupotea kwa Sh21 bilioni, hayasimamiwi na wizara yake.
Alisema mabwawa hayo, ambayo yanapaswa kujengwa katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, yanasimamiwa na Halmashauri ya Ustawi wa eneo la Bonde Kerio (KVDA), ambayo iko chini ya Wizara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mamlaka za Kiamaeneo.
“Baadhi ya vyombo vya habari zimetoa madai yasiyo na ukweli kwamba mimi ni miongoni mwa maafisa wa serikali walioitwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhojiwa kufuatia madai ya kupotea kwa mabilioni ya fedha. Ningependa kuifahamisha kamati hii kwamba mabwawa hayo yanasimamiwa na Wizara ya Afrika Mashariki,” akasema.
Bw Chelugui aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Maara, Kareke Mbiuki kwamba jumla ya mabwawa 57 yanaendelea kujengwa nchini na yanasimamiwa na wizara nne tofauti, ambazo ni ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kawi, Kilimo na Maji.
“Kwa hivyo, ningependa kuomba kamati hii kuanzisha mazungumzo na asasi mbalimbali za serikali ili kuiwezesha wizara yangu kusimamia ujenzi wa mabwawa yote nchini. Maji ni rasilimali muhimu zaidi nchini na inafaa kusimamiwa na wizara moja kwa niaba ya wizara zote,’ akasema.
Bw Chelugui aliwahakikishia wabunge kwamba ujenzi wa bwawa la Itare katika Kaunti ya Nakuru utaendelea, licha ya mwanakandarasi aliyepewa kazi hizo kutangaza kuwa amefilisika.
“Kazi iliyosalia katika ujenzi wa bwawa la Itare itapewa wanandakasi wengine, kwa sababu mwanakandarasi kutoka Italia aliyepewa kazi hiyo ametangaza kufilisika. Hata hivyo, hatutakatiza kandarasi ya kampuni hiyo ya CMC di Ravenna,” akaeleza waziri huyo.
Hata hivyo, wabunge Chachu Ganya (Horr Kaskazini), Hillary Kosgey (Kipkelion Magharibi) na Charles Ongondo Were (Kasipul) walitilia shaka maelezo ya Bw Chelugui wakielezea hofu kwamba huenda mradi huo ukakwama.
“Naona pesa za umma zikipotea katika mradi huu. Mbona serikali ilipeana kandarasi ya mradi muhimu kama huu kwa kampuni ambayo haina uwezo kukamilisha kazi?” akauliza Bw Kosgey.