TAHARIRI: Serikali itimize ahadi ya vitabu kwa shule
NA MHARIRI
AHADI ya serikali ya kutoa vitabu teule vya fasihi (set books) bila malipo kwa kila mwanafunzi wa shule za sekondari za umma imesalia ndoto tu.
Ni jambo la kusikitisha kuona zaidi ya wanafunzi 10 wakitumia kitabu kimoja cha fasihi shuleni ilhali serikali ilisema itasambaza vitabu hivyo mwanzo wa mwaka huu.
Kimsingi, vitabu hivyo vya fasihi vinapaswa kusambazwa kwa wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne mapema muhula ukianza ili kujiandaa kwa Mtihani wa Kitaifa wa Sekondari (KCSE).
Wasimamizi wa shule za umma za upili walikuwa wakitarajia kupokea vitabu hivyo Januari mwaka huu baada ya shule kufunguliwa kama serikali ilivyokuwa imeahidi.
Kinyume cha matarajio yao, wakuu hao wamejipata katika njia panda miezi miwili baada ya mwanafunzi kuingia shuleni.
Baadhi ya shule nyingi nchini haziwezi kununua vitabu, kalamu, chaki na vifaa vingi vingine muhimu vya kufanikisha shughuli za ufunzaji, na haifai kwa serikali kujitia hamnazo kuhusiana na ahadi yake.
Wazazi nao wanaendelea kulia kuhusu mzigo wa karo na haifai kwa serikali kutarajia wazazi wagharamie ununuzi wa vitabu hivyo.
Ikumbukwe kwamba, ni serikali yenyewe inayopanga mitaala na ratiba za kufunga na kufungua shule na bila shaka mipango hii ya inafaa kwenda sambamba na masomo ya vitabu vya fasihi.
Ni dhahiri kwamba utepetevu huu wa serikali utaathiri ubora wa elimu pakubwa kiasi cha kusababisha matokeo mabaya ya mtihani, haswa katika mitahani ya Kiswahili na Kiingereza.
Ni sharti serikali ifahamu kwamba, haki ya kila mwanafunzi kupata elimu bora inalindwa na katiba ya nchi hii, na kuchelewesha vitabu vya fasihi ni ukiukaji wa haki hiyo.
Tayari Wizara ya Elimu inakumbwa na sakata ya ununuzi wa vitabu vingi kupita kiasi na haifai kuruhusu kashfa nyingine ya vitabu.
Mitihani ya lugha za Kiswahili na Kiingereza ni muhimu sana kwa sekta zote za uchumi na serikali haipaswi kuwa mstari wa kwanza kuwa kuzuizi cha ufanisi wa mitihani hiyo.
Ni matumaini yetu kuwa serikali itasambaza vitabu hivyo haraka iwezekanavyo.