Afurushwa nyumbani kwa kuzaa na babake mzazi
Na KAZUNGU SAMUEL
FURAHA ya kujifungua mtoto salama katika hospitali kuu ya mkoa wa Pwani, jijini Mombasa, imegeuka karaha kwa Mary kufuatia hofu ya kukataliwa kurejea nyumbani kwao kaunti ya Vihiga.
Mary alifukuzwa nyumbani kwao Agosti mwaka jana baada ya kufichua kuwa alikuwa mja mzito na mhusika ni babake wa kambo Bw Elphas Anyanda.
Ufichuzi huo ulisababisha kutimuliwa kwake kwa sababu tamaduni za jamii ya Waluhya haziruhusu mtoto aliyetokana na unajisi kuishi katika jamii. Msichana huyo pia hawezi kuruhusiwa kutangamana na wanajamii wengine.
Msichana huyo wa darasa la sita alipachikwa mimba usiku wa Aprili 10 baada ya kunajisiwa na mwanamume huyo aliyemtegemea kumpa malezi ya baba ambayo hakuwahi kuyapata.
“Ilikuwa saa tano usiku wakati baba huyo alinipeleka kulala kwenye nyumba ya nyanyangu ndipo aliponigeukia na kunishikia kisu. Alininajisi na kunitishia kuniuwa iwapo ningefichua siri hiyo,” akasema Mary.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Mary alisema kisa hicho kilitokea siku ambayo mamake mzazi alikuwa amesafiri.
Nyanyake alikuwa pia amesafiri na alibaki na babake huyo wa kambo. Baada ya mamake kurudi, Mary alikuwa na wasiwasi kuishi kwenye boma hilo na akaamua kuishi katika nyumba za marafiki na majirani.
“Baada ya kukaa kwa muda wa wiki moja mbali na nyumbani kwa sababu ya uoga, rafikiye mamangu alikuja nyumbani humo na wakanichukua kunipeleka polisi,” akasema.
Mari alipelekwa kwenye kituo cha polisi cha Luanda pamoja na rafikiye ambaye aliachiliwa. Aidha, alidai alikaa katika kituo hicho cha polisi kwa muda wa siku tatu.
“Baada ya siku tatu niliamua kueleza maafisa wa polisi kuwa nilikuwa silali nyumbani baada ya kupachikwa mimba na babangu wa kambo. Familia ilipogundua hilo walimtorosha babangu na kunitoa mimi kituoni,” akasema.
Alipotolewa kwenye kituo hicho, Mary alifukuzwa na mamake akamjulisha mamake mdogo jijini Mombasa kuhusiana na matukio hayo.
Mamake huyo mdogo alielekeza Mary apelekwe Mombasa ambapo atajifungua na kupinga mapendekezo ya mamake kuwa mimba hiyo itibuliwe.
Msichana huyo ambaye alichelewa kuzaa kwani alitarajiwa kujifungua Disemba, alipelekwa katika hospitali ya CPGH wiki hii ambapo alijifungua mtoto wa kiume.
Hata hivyo, Mary hataki mtoto huyo. “Siwezi kumchukua mtoto huyu kwa sababu siruhusiwi kitamaduni. Na vile vile nataka kurudi shule kusoma,” akasema.
Mamake mdogo ambaye anaishi eneo la Changamwe alisema hawezi kukubali kuishi na mtoto huyo kwa sababu ya tamaduni.
Alisema kwa sababu ni mtoto wa kiume, iwapo atalelewa kwenye familia basi hatachukua muda mrefu kabla afariki, kulingana na mienendo ya tamaduni zao.
“Hatuwezi kulea mtoto huyo, afadhali akalelewe kwenye makao ya watoto. Mimi pia sina muda wa kulea huyu mtoto kwa sababu nipo kazini. Na Mary hapa anafaa arudi shule. Sitaki kuchukua mtoto alafu nimuache ateseke. Roho yangu haiwezi kuniruhusu,” akasema.
Tayari wawili hao wameanza mipango ya kupeleka mtoto huyo katika makao ya kutunza watoto wadogo.