Uhuru atakiwa apuuze Ajenda 4 Kuu ili kuzima ufisadi kwanza
Na MARY WAMBUI
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo amemtaka Rais Uhuru Kenyatta, aweke kando utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu na kuazimia kuwacha sifa bora ya kupambana na ufisadi.
Bw Kabogo anaungana na wanasiasa wengine ambao pia wamependekeza hilo kwa Rais.
Alionya kuwa kama Rais hatafanikiwa kupambana na ufisadi atakapokamilisha hatamu yake ya uongozi, atastaafu bila kufanikiwa na chochote.
“Nchi hii inataabika sana kwa sababu ya ufisadi. Tunamwambia Rais, usiwe na hofu kuhusu ajenda nne. Jishughulishe na ajenda moja ambayo ni kupambana na ufisadi,” akasema.
Aliongeza kwamba ufisadi hauhusiani na kabila wala dini bali ni kitendo kinachoendelezwa na watu ambao hutumia mali wanayopora peke yao wanavyotaka hata bila kuhusisha wake wao.
“Ni mtu, hata si na mke wake. Huwa anakula mwenyewe vile anavyopenda,” akasema Bw Kabogo.
Alisema hayo wakati wa misa ya wafu ya marehemu, Bw Michael Matawa Muchangi, ambaye alikuwa kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Malindi, katika Kanisa Katoliki la St Paul eneo la Mukuyu, Ruitu.
Kulingana naye, ufisadi mkubwa unaoshuhudiwa nchini husababishwa na Wakenya wachache ambao wana ulafi wa mali ya umma.