Tumefanikiwa asilimia 99 kufuatilia wagonjwa wa Ebola – Serikali
SERIKALI imesema imefaulu kwa asilimia 99 kuwafuatilia watu waliotagusana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini pamoja na jamaa zao, huku idadi ya visa vilivyothibitishwa vikifikia saba.
Kati ya visa hivyo, vinne ni vya watu ambao tayari walikuwa wametengwa kwa ajili ya kufuatiliwa. Maambukizi hayo yamesababisha kifo kimoja hadi sasa.
Katibu wa Idara ya Afya ya Umma Mary Muthoni alisema maafisa wa afya wameimarisha ufuatiliaji na hatua za kuzuia ugonjwa huo usisambae katika jamii.
Wizara ya Afya pia imezitaka serikali za kaunti kuandaa vituo vya karantini iwapo idadi ya maambukizi itaongezeka.
Vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi vimetumwa katika maeneo yaliyo hatarini, hasa kaunti zinazopakana na nchi jirani na sehemu kuu za kuingilia nchini.
Bi Muthoni aliwataka Wakenya kuzingatia usafi, kuepuka kugusana na majimaji ya mwili yanayoweza kuwa na virusi na kuripoti watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo haraka.
Alisisitiza umuhimu wa kunawa mikono, kuepuka ngono bila kinga na watu walioambukizwa au wanaoshukiwa kuwa na Ebola, pamoja na kuepuka kupeana mikono na kupigana busu na wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi.
Serikali imewahimiza wananchi kutokuwa na hofu, ikisema kugundua ugonjwa mapema na kupata matibabu yanayofaa ni muhimu katika kuudhibiti. Wizara pia imehusisha asasi za kidini katika kampeni ya kuelimisha umma na kupambana na habari potovu.
Viongozi wa makanisa wametakiwa kuwahimiza waumini kuripoti dalili za ugonjwa mapema, kuzingatia usafi na kuepuka kugusa majimaji ya mwili wa wagonjwa au wanyama wa porini walio wagonjwa au waliokufa.
Nairobi imeitenga Hospitali ya Mama Margaret Uhuru Kenyatta iliyoko Kariobangi Kaskazini kuwa kituo cha karantini.
Gavana Johnson Sakaja alisema kaunti imeimarisha ufuatiliaji na inashirikiana na serikali ya kitaifa kuwalinda wakazi.
Alisema wahudumu wa afya wamepewa mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga, kuwahudumia wagonjwa kwa usalama na kusafisha magari ya wagonjwa ili kuzuia maambukizi.