Ruto, Natembeya wapimana ubabe kuhusu maendeleo
MVUTANO wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya umechacha huku washirika wao wakipigana vikali kuhusu miradi ya maendeleo na uchaguzi wa 2027.
Bw Natembeya ametaka ufafanuzi kuhusu ufadhili wa miradi iliyotangazwa na Rais, akitishia kuzuia mradi wa hospitali ya Sh1 bilioni huku akipinga kile anachokitaja kuwa serikali ya kitaifa kujipatia sifa kwa miradi ya kaunti.
Mvutano huo uliongezeka baada ya Rais kutembelea kaunti hiyo mara kadhaa wiki iliyopita, akimkosoa gavana kuhusu huduma za afya na kuwatambulisha wanasiasa wanaoweza kumpinga katika uchaguzi ujao.
Rais alielezea Hospitali ya Rufaa ya Wamalwa Kijana kama hatari kwa wagonjwa, akidai imepewa jina la “Shakahola” kwa sababu wagonjwa wanaoenda kutafuta matibabu humo hawarudi wakiwa hai.
“Viongozi wanapaswa kupanga kuhusu afya, wala si mazishi ya wananchi wao,” alisema Dkt Ruto, akitangaza kujenga hospitali mpya ya vitanda 300 ndani ya miezi minane.
Hata hivyo, Bw Natembeya amehoji umuhimu wa kujenga hospitali nyingine bila kuweka wazi mipango ya ufadhili, akisema vituo vilivyopo vinapaswa kuimarishwa.
Washirika wa Rais, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen na Seneta wa Trans Nzoia Allan Chesang, wamemkosoa gavana na kuahidi kuwarai wapigakura kumwondoa mamlakani 2027.
Rais pia aliwatambulisha Mbunge wa Kiminini Kakai Bisau, aliyekuwa mbunge Chris Wamalwa na mwakilishi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa Susan Nakhumicha kama viongozi wanaoweza kushindana na Bw Natembeya.
Mgogoro mwingine unahusu Uwanja wa Kitale ambao ujenzi wake umekwama. Rais alisema serikali ya kitaifa itachukua jukumu la kuukamilisha.
“Ingawa nimejenga viwanja 32 kote nchini, uwanja wenu umekwama kwa miaka mingi. Gavana wenu ameshindwa kuukamilisha, nami nitachukua jukumu la kuumaliza,” akasema Rais.
Bw Natembeya alijibu kwamba alikuwa ameidhinisha mazungumzo na maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya kuhusu kukamilisha mradi huo kwa fedha za serikali ya kitaifa. Alidai mradi haujaanza kwa sababu amekataa kujipendekeza kisiasa kwa Rais.
Kuhusu soko la kisasa la Masinde Muliro mjini Kitale, Dkt Ruto alisema serikali ya kitaifa imetumia karibu Sh1 bilioni kulijenga na akaagiza wafanyabiashara 1,500 walioathiriwa na ujenzi wapewe kipaumbele katika ugawaji wa vibanda. Kila mmoja alipewa Sh10,000 za kuendeleza biashara yake.
Bw Natembeya ameapa kufuatilia ugawaji huo ili kuhakikisha wafanyabiashara wa eneo hilo hawabaguliwi na watu kutoka nje.
Mvutano umeongezeka zaidi baada ya walinzi wa gavana kuondolewa kwa mara ya pili. Ameitaka Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kueleza sababu za hatua hiyo, akisema usalama ni haki wala si mapendeleo.
Gavana amehusisha hatua hiyo na tofauti zake za kisiasa na serikali ya kitaifa, ingawa madai hayo hayajathibitishwa kwa njia huru.
Vuta nikuvute ilidhihirika pia katika mazishi ya Afisa Mkuu Msaidizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi Lazarus Simiyu Opicho huko Maili Saba ambapo Bw Natembeya na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna walikutana na washirika wa Rais.
Kaulimbiu za “Wantam” zilivuruga shughuli na kuzuia baadhi ya viongozi wa upinzani kuhutubia waombolezaji.
Baadaye, polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya mkutano wa viongozi wa upinzani mjini Kitale.
Huduma ya Kitaifa ya Polisi ilisema maafisa wawili walijeruhiwa na magari mawili ya serikali kuharibiwa, huku uchunguzi ukianzishwa.