MFUMO mpya wa elimu; 2-6-6-3 katika kaunti ya Nakuru tayari unaonekana umeanza kuzaa matunda katika baadhi ya shule za msingi tangu uanze kutekelezwa nchini na Wizara ya Elimu.
Shule ya msingi ya Radiance iliyoko eneo la Lanet Nakuru Mashariki, imekumbatia mfumo huu na tayari wanafunzi wanaendelea kupata mafunzo ya masomo ya kimsingi, jambo ambalo walimu pamoja na wanafunzi wanaeleza linawapa ujuzi mwingi kuliko mfumo unaotazamiwa kupigwa teke wa 8-4-4.
Mkurugezi mkuu wa shule ya Radiance Bi Mercy Njeri Kibe, anasema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto kama ukosefu wa muda wa kutosha, wanafunzi wanafurahia mfumo mpya, jambo ambao unalenga kukuza talanta na si uwezo wa kupita mtihani tu jinsi ilivyo katika mfumo wa sasa wa 8-4-4.
Kulingana naye, mtaala huo pia unalenga kupanua uwezo wa fikira wa wanafunzi badala ya kuzingatia sana yaliyo katika silabasi. Baadhi ya masomo yanayochangamkiwa sana na wanafunzi ni upishi, urembo na mapambo, uchoraji, uhandisi na masomo ya kutoa huduma za kwanza.
Changamoto
Bi Kibe anasema kuwa haijakuwa safari rahisi kwake na walimu kufikia kiwango ambacho wamefikia sasa ila ni mazao ya kujituma na kujikakamua vilivyo. “Tuna mafunzo ya upishi na wanafunzi wetu wameonyesha ubora wao katika masomo hayo. Wanafunzi wa darasa la nne, tano na sita sasa wana uwezo wa kupika vyakula kadha kama vile chapati, mandazi, mahamri na pilau,” Bi Kibe Akaeleza.
Katika ziara ya Taifa Leoshuleni humo, tulibaini kwamba wanafunzi wa darasa la tatu wanafundishwa mapishi na wenzao wa madarasa ya juu.
Baadhi ya mambo ya kimsingi wanayojifunza ni kuiosha mikono yao kabla ya kujitosa jikoni kuandaa mlo wanaoupenda.
Vilevile wao hupata mafunzo ya jinsi ya kuzingatia viwango vya juu vya usafi wakati wa upishi.
Walimu huhakikisha kwamba wanafunzi wote wamevalia sare zinazohitajika kabla ya kujitosa katika somo lolote lile ambalo huhitaji wao kujishughulisha kwa vitendo.