HabariSiasa

Nasaidia Uhuru kuendesha serikali – Raila

March 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga alisema Alhamisi anasaidiana na Rais Uhuru Kenyatta kuendesha Serikali kwa mujibu wa mwafaka wao wa maelewano mnamo Machi 9, mwaka 2018.

Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Kameme FM jana, Bw Odinga alisema ni kutokana na hali hiyo ambapo amekuwa akiwaita mawaziri na maafisa wengine wa Serikali katika afisi yake kushauriana nao kuhusu masuala ya wizara zao.

“Ninapowaita mawaziri afisini mwangu ni katika mkakati wa serikali kuwashirikisha wananchi katika uongozi wa nchi, na mimi nikiwa mmoja wao. Wakati mwingine huwa nawapa ushauri kuhusu namna ya kuendesha serikali kwa kuwa nimehudumu serikalini kwa muda mrefu,” akasema Bw Odinga.

Miongoni mwa mawaziri ambao wamefika katika afisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi ni Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Eugene Wamalwa (Maji), Peter Munya (Biashara na Viwanda), Margaret Kobia (Utumishi wa Umma) na Waziri Msaidizi Rachael Shebesh.

Rais mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshiskedi pia alimtembelea Bw Odinga katika afisi yake kabla ya kuzuru Ikulu kuonana na Rais Kenyatta mwezi uliopita.

Bw Odinga pia alialikwa katika Ikulu na Rais Kenyatta kuwapokea Rais Alain Bersett wa Uswizi na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May walipozuru Kenya mwaka uliopita.

Amekuwa pia akitembelewa na maafisa wakuu serikalini akiwemo Afisa Mkuu wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), Nancy Macharia.

Kwenye ziara yake mwezi Desemba katika Kaunti ya Kisumu kuzindua mpango wa Afya kwa Wote (UHC), Rais Kenyatta alisema Bw Odinga yumo ndani ya utawala wake.

“Ningependa kuwaambia wakazi wote kwamba ‘Jakom’ yuko ndani ya serikali,” akasema Rais Kenyatta, huku akishangiliwa na mamia ya wakazi.

Hata hivyo, Bw Odinga alijitetea vikali dhidi ya madai ya kuingilia masuala ya serikali ya Jubilee, akishikilia kuwa anashirikishwa tu katika masuala ya uongozi.

Pia alijitetea kuhusu madai kuwa ana njama ya kusambaratisha chama cha Jubilee, akisema kuwa anasingiziwa bure na mahasimu wake kisiasa.

Baadhi ya wabunge wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakimlaumu Bw Odinga kwa madai ya kutumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kusambaratisha umoja wa chama hicho.

Wabunge hao wamekuwa wakidai kwamba lengo lake ni kukigawanya chama hicho ili kuzima ndoto ya Dkt Ruto kushinda urais 2022.