Vita kati ya Ruto na Raila vyazidi kupamba moto
Na PETER MBURU
NAIBU Rais William Ruto Alhamisi alimrushia makombora kinara wa ODM Raila Odinga kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi huku akishikilia kuwa idara za kupambana na ufisadi zimefeli kwa kukubali kupewa masharti ya kulenga watu fulani.
Akizungumza alipofunga rasmi Kongamano la Ugatuzi lililoandaliwa katika Kaunti ya Kirinyaga, Dkt Ruto alimlaumu Bw Odinga kwa kuingilia utendakazi wa mamlaka na tume za kikatiba, akisema hilo limelemaza vita dhidi ya ufisadi.
Naibu Rais alidai kumekuwa na lengo fiche katika vita hivyo na usambazaji wa habari za uongo ili kuchafulia watu majina.
“Hatari kubwa zaidi kwa vita dhidi ya ufisadi ni kushtaki watu kwa ubaguzi, kulenga watu na miradi fulani kwenye chunguzi hizo, kusambaza uvumi na uongo na kuvuruga ukweli,” akasema Dkt Ruto.
Matamshi hayo yalikuja siku chache baada ya kukosoa habari za Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuwa kiwango cha pesa ambazo zimefujwa katika mradi wa mabwawa mawili eneo la Bonde la Ufa ni Sh7 bilioni badala ya Sh20 bilioni ilivyosema idara hiyo.
Aliwalaumu watu aliosema wanaweka siasa katika vita dhidi ya ufisadi, akisema ndio kikwazo kikuu kwa vita hivyo. Dkt Ruto alisema hawezi kuwasikiza watu ambao wenyewe si safi wakimzomea kuhusu masuala ya ufisadi na maadili.
“Ni wanasiasa tapeli wanaojulikana na ambao maneno yao hayana maana yoyote, wala hawastahiki na hawana maadili ya kumzomea yeyote kuhusu masuala ya ufisadi na maadili.”
Naibu Rais alisisitiza kuwa “sharti tupigane vita dhidi ya ufisadi na sharti tupigane tukitumia silaha zinazofaa ili kufaulu kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kufaulu.”
Akimjibu aliyekuwa Waziri Mkuu kwa maswali yake kuhusu kinachomsukuma kuzungumzia zaidi suala la sakata ya ujenzi wa mabwawa, Dkt Ruto alimtaka kiongozi huyo kuripoti kwa mamlaka zinazohusika na kuchunguza ufisadi ikiwa anadhani kuna kitu cha kuchunguzwa.
“Alipofungua kongamano hili, Rais aliwataka wote ambao wanamjua mtu ambaye ameiba ama kufuja pesa za umma kuwasilisha malalamishi yao kwa taasisi za kuchunguza badala ya kupiga kelele kwenye matanga na hafla nyingine.
“Ninafuatilia masuala ya mabwawa kwani ilikuwa moja kati ya sera ambazo tuliahidi katika chama cha Jubilee kuwa, katika miaka mitano tutajenga mabwawa 57.
“Swali ambalo ninaulizwa ni sawa tu na fisi kumuuliza mchungaji kwanini analinda mifugo wake na kwanini anajua idadi ya mifugo hao,” Naibu Rais akaendelea. Dkt Ruto alishangaa ni kwa nini Bw Odinga analalamika mbele ya umma kuhusu visa vingi lakini hajafika katika mamlaka za kufanya uchunguzi kuwasilisha ripoti na ushahidi.
Kulingana na Naibu Rais, madai ya Bw Odinga ni vita anavyompiga kwa kuwa anafahamu kuwa watapambana naye katika uchaguzi mkuu wa 2022.
“Katika uchaguzi uliopita ulisema washindani wako waliiba pesa za Eurobond, sasa unamlaumu mtu ambaye unadhani atakuwa mshindani wako kuwa ameiba pesa za ujenzi wa mabwawa na ukiulizwa ‘mkubwa huu ushahidi utapeleka Karura (DCI) ama EACC’ unasema ‘hapana najua nyinyi ni wezi kwa sababu nilipigiwa simu na baba mtakatifu’” akasema.