Wabunge watatu wamkemea Ruto kwa kumuita Raila 'tapeli mkuu wa kisiasa'
Na PETER MBURU
WABUNGE wamezidi kutofautiana kuhusiana na vita vya maneno kisiasa ambavyo vinaendelea baina ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, kuhusu jinsi vita dhidi ya ufisadi vinaendeshwa, na harakati za kuunganisha taifa.
Ijumaa wabunge Mark Nyamita (Uriri), Anthony Oluoch (Mathare) na Abdulswamad Nassir (Mvita) walimkashifu Dkt Ruto kwa kumvamia Bw Odinga kuwa hana mamlaka ya kimaadili kuzomea yeyote kuhusu ufisadi, wakisema yeye ndiye amepotoka.
Wakizungumza na wanahabari bungeni, wabunge hao walimlaumu Naibu Rais wakimtaja kuwa ndiye kikwazo katika vita dhidi ya ufisadi na harakati za kuunganishwa kwa Wakenya.
Viongozi hao walisema Rais Uhuru Kenyatta ameonyesha kila dalili kuwa hataki kumhusisha Dkt Ruto kwenye vita dhidi ya ufisadi ili asivichafue, japo kila mara anajialika katika suala hilo.
“Hafai kukanganya habari za maafisa wanaohudumu katika serikali. Huko ni kuingilia uchunguzi anapovamia idara za DCI na EACC zikifanya kazi yake,” akasema Bw Nyamita.
Akimjibu kuhusu matamshi yake kuwa yeye ndiye ‘mchungaji’ wa miradi ya serikali na mhasibu, Bw Oluoch alisema Rais hana imani na naibu wake na ndipo amekuwa akisisitiza kuwa kazi ya kupigana na ufisadi ni ya mamlaka za EACC na DCI.
“Rais amesema kuwa mchungaji na mtu aliyejukumiwa uhasibu na kujua kile kimeibiwa ama hakijaibiwa ni DCI.”
Kuzingatia ukabila
Viongozi hao walimtaka Naibu Rais kukoma kusema kuna watu wanaolengwa katika vita hivyo, kwani serikali ikiundwa walizingatia ukabila badala ya ufaafu wa watu, kuwapa kazi.
Lakini viongozi wengine kama mbunge wa Kandara Alice Wahome nao walimlaumu Bw Odinga kuwa ndiye kikwazo kwa lengo la muafaka baina yake na Rais, ambalo lilikuwa kuunganisha taifa.
“Hatari kubwa zaidi kwa hatua ya kuunganisha taifa ni Raila Odinga, hili lilikuwa wazi alipohutubia kongamano la ugatuzi. Na sasa inakuwa wazi kuwa dhana ya kuunganisha taifa ni mpango wa kupeperusha kampeni kuhusu uchaguzi wa 2022,” akasema Bi Wahome.