UMBEA: Kumnyima unyumba, ni kukaribisha vidudumtu kwenye ndoa yenu!
Na SIZARINA HAMISI
NINAJUA wapo akina dada hodari wa kutumia tendo la ndoa kama silaha ya kuwaadhibu waume ama wapenzi wao.
Kwamba pale anapohitaji kitu fulani kutoka kwa mwenzake, basi atatumia burudani kama mbinu ya kupata akitakacho.
Vilevile pale anapokasirishwa na mwenzake, hutumia burudani pia kumuadhibu mwenzake hasa kwa kumkatalia ama kumpangia.
Hali hii huwa tata zaidi pale ambapo mwanamke anakuwa mjuzi wa burudani kiasi cha kumpagawisha mwenzake. Kwani ujuzi huo wakati mwingine hutumika kwa jinsi ambayo haina faida bali karaha.
Unyumba ni kiunganishi adimu kwenye uhusiano, baadhi ya wapendanao hasa wanawake hupenda kutumia nafasi hiyo kuwanyanyasa wenzao.
Wanageuza unyumba kuwa fimbo ya kuwatandika waume zao.
Mwanamke wa aina hii anaona ili kumkomoa mumewe ama mpenzi wake kutokana na kosa alilotendewa, atamnyima unyumba.
Anaamini ni silaha yenye nguvu kubwa.
Anadhani kwamba mwanamume aliyekamilika, ni lazima atarudi kwake akitaka huduma hiyo muhimu.
Kukata kiu
Atahangaika huku na kule akiwa faragha ili mradi tu akate kiu yake.
Wanaamini wanaume si wavumilivu. Watahangaika, mwisho wa siku watahitaji tu huruma ya mkewe.
Penzi wanaligeuza kama hisani. Yeye ndiye mmiliki wa tendo hilo. Akitaka atatenda, asipotaka basi hakuna kitakachoeleweka.
Wanaamini kwamba ili mwanamume apewe, inabidi awe mpole. Ajishushe.
Kama alikosea, anapaswa kuomba msamaha, asamehewe ndipo mambo yaendelee.
Vinginevyo ataishia kulala mzungu wa nne.
Iwapo hii ni tabia yako, mazoea yako, tambua kwamba tendo la ndoa lina umuhimu wake. Kwa namna moja au nyingine linakamilisha maana nzima ya mapenzi.
Ni kama vile kachumbari kwenye pilau. Si kwamba pilau hailiki bila kachumbari lakini ikiwepo, utamu unakamilika.
Ili kuleta ustawi wa penzi ama ndoa, mwanamke ana wajibu wa kutuliza kiu ya mume wake, hali kadhalika mwanaume anao wajibu wa kunyamazisha kiu ya mkewe.
Mmoja kati yenu anapolifanya chini ya kiwango, humweka mwenzake njia panda, yaani kumtia kishawishi cha kujaribu kule ama huko.
Sio busara kutumia unyumba kama silaha ya kumchapa mwenzako pale anapokosea.
Ni bora ukamuadhibu kwa mambo mengine lakini si unyumba.
Burudani ni kiunganishi muhimu, kinapokosekana, madhara yake ni makubwa na usaliti huanzia hapo.
Binadamu aweza kuchoka
Kumnyima mwenzako unyumba, ni kukaribisha vidudumtu kwenye ndoa yenu. Atavumilia, ila ni binadamu anaweza kuchoka.
Anaweza kutafuta jinsi ya kufanya. Akiifanya, akinogewa, umuhimu wako kwake huishia hapo.
Atakulinganisha wewe na yule aliyechepuka naye. Ataona amepata tiba sahihi.
Ni rahisi kukufanya wewe ni mlezi wa familia. Baadaye mwanamke naye atagundua, naye ataona njia nzuri ya kumkabili ni kujibu mapigo.
Hapo ndiyo kunakuwa hakuna tena uhusiano madhubuti. Kama ni ndoa itakuwa rehani. Muda wowote inaweza kuvunjika, kila mmoja akachukua njia yake.
Halafu wapo wale wanawake ambao wanadhani kumpa unyumba mumewe ni sawa na kumpa zawadi, kwamba wanafanya hivyo kwa faida ya mume na kwamba yeye hafaidiki lolote.
Ni muhimu umfurahishe mumeo ukiona ni wajibu wako na wala sio kwamba unatenda fadhila kwake. Uone kwamba unayo kila sababu ya kumpa maana wewe ndiye mtu sahihi.
Wewe ndio unapaswa kumtimizia mahitaji yake ya kimwili, kiakili na hata kifikra.
Kama amekosea, kasirika, nuna na baadaye hasira zikiisha, mueleze pale alipokukwaza. Kama binadamu, atapima na ataelewa makosa aliyoyafanya.
Hata kama mna ugomvi, linapokuja suala la unyumba hupaswi kulifanyia mzaha maana ni hatari kwa mustakabali wa penzi lenu.
Ujue unaposema wa nini, wapo wenzako wanaojiuliza watampata lini.