Michezo

Emery hawezi kudhibiti mastaa kikosini – Salgado

March 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

NYOTA wa zamani wa Real Madrid  Michel Salgado amesema kwamba kocha wa Arsenal Unai Emery bado hana uzoefu wa kuongoza timu ambayo ina wachezaji nyota wenye majina ‘makubwa’ kama makocha wengine watajika wanaongoza klabu za hadhi barani Uropa.

Huku akimsifia kwa kuongoza Arsenal kuwashinda watani wao wa jadi Manchester United 2-0 Jumapili Machi 11 ugani Emirates, Salgado alisema kwamba ilikuwa vigumu kwa kocha huyo kushughulikia hali ya Mesut Ozil anayedaiwa hawaelewani naye timuni. Ozil amekuwa akilishwa benchi kwenye mechi za nyuma za Arsenal ingawa Jumapili alianza mechi dhidi ya The Red Devils na kungáa sana.

“Emery huhitaji kikosi ambacho kina wachezaji ambao anaweza kuwadhibiti msimu mzima. Hawezi kupambana na mchezaji kama Ozil ambaye amekuwa na taaluma ya kupiga mfano kwenye taaluma ya soka kuliko ukufunzi wa wake,”

“Arsenal kwa sasa ina kikosi cha wachezaji wazuri ingawa hawana wachezaji wenye majina kama Ozil na lazima Emery ajifunze kukabiliana na presha zinazoandamana na uwepo wa wachezaji kama hao timuni,” akasema Salgado.

Katika mechi dhidi ya Manchester United, kocha huyo aliamua kumpanga Ozil na Aaron Ramsey kwenye safu ya kiungo  huku Alexandre Lacazette na Pierre- Emerick Aubameyang katika safu ya ushambulizi. Mabao ya Arsenal yalifungwa na Xhaka na Aubameyang.

Kupangwa kwa kikosi hicho hivyo kilichangia ushindi  huo na kufufua matumaini ya Arsenal kutinga nne bora na kuimarisha uwezo wao wa kufuzu kushiriki Klabu bingwa Barani  Uropa msimu ujao wa 2019/ 2020.

Hata hivyo Salgado alikiri kwamba mkufunzi huyo wa zamani wa PSG, Sevilla ameridhisha katika msimu wake wa kwanza Arsenal na anaweza kutambisha timu hiyo akipewa muda na sapoti anayohitaji kutoka kwa uongozi wa Arsenal.