• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Mbunge aitaka serikali kukabiliana na mafisadi bila huruma

Mbunge aitaka serikali kukabiliana na mafisadi bila huruma

Na LAWRENCE ONGARO
SERIKALI ni sharti ipambane na ufisadi kwa vyovyote vile kwani vimekithiri mipaka, amesema kiongozi.
Mbunge wa Thika, Mhandisi  Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema Jumapili kwamba kutoka serikali kuu hadi zile za kaunti ufisadi umekithiri kiasi kwamba ni sharti serikali ijutume kwa nguvu zake zote ipambane na donda hili.
“Ufisadi umegeuzwa kama mtindo wa kila siku na ni kawaida wao kupora mali. Huu ndiyo wakati wa kushughulikia tatizo hilio,” alisema Bw Wainaina mnamo Jumapili.
Alisema kila siku tunapotazama vyombo vya habari tunashuhudia maswala ya ufisadi yakiangaziwa.
Aliyasema hayo alipofanya mkutano na dhehebu la Akorino la Aroti Pillar, ambapo waumini kutoka kaunti nzima ya Kiambu walipata fursa.
Wafuasi hao wa Akorino walijumuika katika Uwanja wa Thika Stadium lengo lao kuu likiwa ni  kutaka kutambulika katika uongozi wa kitaifa na ule wa Kaunti ya Kiambu.
Wakiongozwa na Askofu wao kutoka Kaunti Ndogo ya Ruiru, Bw Josphat Gathua, walisema hawatakubali kuwekwa katika mstari wa nyuma wakati wa kupeana mamlaka au kugawana mamlaka.
Walisema dhehebu lao litafanya juu chini kuona ya kwamba wafuasi wake wanaunga mkono ajenda kuu nne za serikali kwa sababu mpango huo ndiyo utakaobainisha maono ya Rais Uhuru Kenyatta baada ya miaka mitatu na nusu.
“Sisi kama dhehebu la Akorino tunajieleza kwa sauti moja ya kwamba ni sharti tutambulike kama viongozi wengine,” alisema Bw Gathua.
Alisema ya kwamba katika nchi nzima ya Kenya wana matawi yapatayo 25 na wametoa kauli ya kwamba watakuwa  wakizungumza kwa sauti moja ili ujumbe wao uweze kufika pahala panapostahili.
Bw Wainaina kwa upande wake alisema wananchi wa Kenya wanapata shida ya kibiashara.
Zabuni
Walisema wao kama dhehebu la Akorino wangetaka pia kupewa zabuni za miradi tofauti ili waweze kujivunia jasho lao la kikazi kama wacha Mungu.
Bw Wainaina alisema bidhaa za mayai na matunda pamoja na maziwa kutoka Afrika Kusini na Uganda yameathiri kwa njia hasi biashara za hapa nchini tena kwa kiwango kikubwa ajabu.
“Ningetaka serikali iwatoze ushuru ada ya juu zaidi ili wapunguze kiwango cha bidhaa zao wanazoleta hapa nchini. Wengi wa wafanyabiashara wameamua kufunga biashara kwa sababu ya kupata hasara wanapouza bidhaa hizo,” alisema Bw Wainaina.
Alitoa mwito kwa vijana na wanawake wajitokeze wazi kuomba fedha za mikopo ya Youth Fund ili waweze kuendesha biashara zao kwa njia inayostahili.
Bw Gathua ambaye ni askofu wa tawi la Ruiru alisema wameamua kwa kauli moja ya kwamba hakuna dhehebu la kikundi chao litakalokubaliwa kuendesha mambo yao bila kupitia kwa wakuu.
Sisi kama viongozi wa kanisa tutakuwa tukishirikiana pamoja kama familia moja ili kufanya mambo tena kwa sauti moja, ” alisema Askofu Gathua.

You can share this post!

VIDUBWASHA: Pochi ya nyaya za chaja (Twelve South CaddySack)

Moto wateketeza soko la Toi, maswali mazito yaibuka

adminleo