• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Keter: Vita dhidi ya ufisadi havilengi jamii ya Wakalenjin

Keter: Vita dhidi ya ufisadi havilengi jamii ya Wakalenjin

W. KIPSANG na FLORA KOECH

MBUNGE wa Nandi Hills Alfred Keter, amewapuuzilia mbali baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka Bonde la Ufa wanaodai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea vinawalenga watu kutoka jamii ya Wakalenjin.

Kulingana na Bw Keter , wale waliohusishwa na sakata za ufisadi wanapaswa kubeba msalaba wao badala ya kuelekeza lawama zao kwa Rais Uhuru Kenyatta na kutafuta kinga ndani ya jamii ya Wakalenjin.

“Watu hawa wakome kabisa kuingiza jina la Rais Kenyatta na jamii nzima ya Wakalenjin katika sakata hii inayowakabili. Wapambane kama watu binafsi,” akasema.

Mbunge wa Baringo Joshua Kandie pia waliwataka viongozi kutoka jamii hiyo waliohusishwa na sakata ya Sh21 bilioni ya mabwawa ya Arror na Kimwarer, kukoma kujitetea kwa kuingiza jina la Wakalenjin katika masaibu yao.

Akiongea katika sherehe ya ufunguzi wa afisi ya Hazina ya Ustawi wa Eneo Bunge (CDF) mjini xxxKabarnet, Bw Keter alielezea hofu kuwa sakata za ufisadi zimeathiri uchumi wa nchi, na kuifanya kutegemea pesa za mkopo kutoka ng’ambo.

“Viongozi wa Rift Valley, wanaolalamika kwa sauti kubwa kwamba jamii ya Wakalenjin ndio wanalengwa katika vita dhidi ya ufisadi, sharti wafahamu kuwa watuhumiwa hawakuiba kwa niaba ya jamii yetu. Walipora kwa manufaa yao na wabebe misalaba yao. Wakome kupiga kelele kuwa kiongozi fulani ya Kalenjin ndiye analengwa,” akasema Bw Keter.

Alisema wakazi wa maeneo ya Arror na Kimwarer ambako mabwawa hayo yalipaswa kujengwa, hawajalipwa ridhaa kwa ardhi yao ilhali watu fulani tayari wamelipwa pesa nyingi na kazi bado haijaaza.

Bw Kandie alihusisha kero la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na umaskini miongoni mwa Wakenya na sakata kadhaa za ufisadi.

“Ufisadi hauna kabila wala chama cha kisiasa. Sote tunapaswa kuungana kukomesha uovu huu ambao unaathiri maendeleo nchini. Ikiwa mtu anashukiwa kupora pesa za umma, anapaswa kujibu mashtaka dhidi yake kama mtu binafsi badala ya kuingiza jamii nzima,” akasema Bw Kandie aliyechanguliwa kwa tiketi ya chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC).

Baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo, akiwemo Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, hata hivyo wanashikilia kuwa vita vya ufisadi vinavyoendelea vinalenga watu kutoka jamii ya Wakalenjin pekee.

Bw Sudi ambaye amejitokeza kama mtetezi sugu wa Naibu Rais William Ruto, alilalamika kuwa watu kutoka jamii ya Wakalenjin wanaoshikilia nyadhifa za juu serikali ndio wanaondolewa afisini kwa tuhuma za ufisadi.

“Walipanga njama ya kushtakiwa kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Kenya Power kwa zabuni ambayo ilitiwa saini na Joseph Njoroge, Katibu wa Wizara ya Kawi,” Bw Sudi akadai.

“Ni wazi kuwa vita vyako dhidi ya ufisadi vinalenga watu kutoka jamii fulani, tofauti na madai yake,” akasema huku akionekana kumlenga Rais Kenyatta.

You can share this post!

Tuliiona ndege ikichomeka ikiwa angani – Mashahidi

Aliyedai Uhuru atafariki Machi 20 aagizwa kupimwa akili

adminleo