Polisi waokoa watoto ndani ya kanisa linalowakataza kwenda shule
Na Hamisi Ngowa
POLISI katika eneo la Likoni Mombasa, mwishoni mwa wiki waliwanusuru watoto wanane, wanawake wawili waliodaiwa kuwa waumini wa kanisa la Bethany linalokataza wafuasi wake kwenda shuleni.
Inadaiwa kuwa polisi walipashwa habari kabla ya kuvamia nyumba hiyo iliyoko eneo la Inuka na kuwapata watoto hao wenye umri kati ya miaka mitatu hadi sita wakiwa katika chumba kimoja.
Katika tukio hilo, polisi pia walifanikiwa kuwatia mbaroni wanawake wawili wanaodaiwa kuwa waumini wa dhehebu la kanisa la Bethany lenye makao yake mjini Malindi.
Inadaiwa kuwa waumini wa kanisa hilo wanapinga elimu ya shule wakidai kuwa hata mitume wa Mungu hawakusoma na ilhali waliweza kuishi vyema kwa kumtumikia Mungu.
Majirani katika mtaa huo waliambia Taifa Leo kuwa watoto hao ambao ni wavulana 5 na wasichana 3 wamekuwa wakiishi na wanawake hao tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa hakuwa na idhini ya kuongea na vyombo vya habari, alisema kiongozi mmoja wa dhehebu hilo kutoka malindi alifika katika kituo cha polisi cha Inuka mara tu baada ya watoto hao pamoja na wanawake hao wawili kukamatwa.
Alisema anashuku kuwa huenda mwanaume huyo ndiye kiongozi wa dhehebu hilo linalopinga waumini wake dhidi ya kwenda shuleni.