Habari Mseto

Kuna uhaba mkubwa wa shule za upili Nairobi na Mombasa – Serikali

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Elimu imelalamikia uhaba wa shule za upili katika Kaunti ya Nairobi na kuutaka uongozi wa kaunti hiyo kupiga jeki mpango wa ujenzi wa shule mpya.

Katibu wa wizara hiyo Belio Kipsang’ Jumanne aliwaambia wabunge kwamba shule za upili katika kaunti ya Nairobi zinaweza kuhudumia wanafunzi 30,000 pekee ilhali jumla ya wanafunzi 55,000 wanahitaji kuhudumiwa.

“Tumeitisha mkutano na uongozi wa kaunti ya Nairobi kwa lengo la kushughulikia tatizo hili,” Dkt Kipsang’ aliambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly.

Katibu huyo aliongeza kuwa kaunti ya Mombasa pia inakabiliwa na tatizo hilo la uhaba wa nafasi katika shule za upili kwa sababu ya uhaba wa shule hizo.

Dkt Kipsang’ alisema tatizo hilo la uhaba wa shule za kutosha za upili katika kaunti hizi zenye idadi kubwa ya watu ni mojawapo ya changamoto kuu inayoathiri utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa na nane (KCPE) wanajiunga na shule za upili.

Kulingana na takwimu kutoka wizara ya elimu jumla ya wanafunzi 920,765 kati ya 1,035,664 waliofanya KCPE 2018 wamejiunga na shule za upili.

Aliyekuwa Waziri wa Elimu Amina Mohamed alisema idadi hiyo inawakilisha asilimia 90 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo mwaka jana.

Kaunti ya Nyeri imeandikisha idadi ya juu zaidi ya wanafunzi waliojiunga na shule za upili ikifuatwa na Siaya, Bomet, Nyandarua, Kajiado, Murang’a , Vihiga, Kisumu na Homa Bay katika usanjari huo.

Kaunti za Taita Taveta, Kilifi, Mombasa, Lamu, Kwale, Tana River, Isiolo na Nairobi ni miongoni mwa kaunti ambazo ziliandikisha idadi ndogo ya wanafunzi waliojiunga na shule za upili.

Katika kaunti ya Nairobi mitaa ya mabanda ndiyo imeandisha idadi ndogo ya wanafunzi waliojiunga na shule za upili mwaka huu.