VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili shuleni St Francis Lare (CHAKILA) mwenge thabiti wa lugha
CHAMA cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Francis Lare, eneo la Njoro, Nakuru (CHAKILA) kiliasisiwa mwanzoni mwa 2012 kwa nia ya kubadilisha mtazamo hasi wa wanafunzi kuhusu somo la Kiswahili, kukuza talanta za wanafunzi katika kazi za kubuni, kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine ili kuboresha na kuimarisha matokeo ya KCSE Kiswahili.
Lengo kuu la kuanzishwa kwa chama ni kuweka wazi umuhimu wa lugha ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi; walione somo hili kuwa dhahabu badala ya adhabu.
Madhumuni mengine yalikuwa ni kustawisha lugha ya Kiswahili shuleni; kuzidisha maarifa ya utafiti katika Kiswahili na kushirikiana na vyama vingine ili kuimarisha matumizi ya Kiswahili.
Chama kimetenga kipindi maalum kila siku ya Jumatano ili kusoma gazeti la Taifa Leo hasa ‘Jarida la Lugha na Elimu’ ili kuinua viwango vya lugha miongoni mwa wanafunzi na walimu wa Kiswahili shuleni.
Mwalimu Mkuu ambaye ni mpenzi wa Kiswahili, Bw Victor Kerama amehakikisha kuwa kuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili na nakala za magazeti ya Taifa Leo maktabani.
Wanachama hukutana kila siku kuanzia saa kumi hadi saa kumi na mbili jioni kujadili masuala mbalimbali kuhusu uandishi wa Insha, Sarufi na Matumizi ya Lugha, Fasihi Simulizi, Ushairi na kuchambua vitabu teule vya Fasihi Andishi.
Chama huandaa vikao maalum mara mbili kila muhula kwa lengo la kuwashirikisha wanachama katika mashindano yanayolenga kubaini upekee wa vipaji vyao katika kughani mashairi, kutamba hadithi, kutunga mashairi na kutangaza habari kutoka gazeti la Taifa Leo.
Bw Kerama ambaye pia ni Mlezi wa Chama, hutoa nasaha za kuwatia motisha kuhusu safari ya usomi kwa jumla na washindi hutuzwa.
Chama kinapania kushiriki na kuchangia makuzi ya Kiswahili kupitia kwa vipindi vya Kiswahili ambavyo hupeperushwa kila wikendi katika vituo mbalimbali vya redio humu nchini.
Kufikia sasa, manufaa ya chama hiki yameonekana kwani wanachama wengi wameendelea kufuzu katika somo la Kiswahili na kuwapiku wenzao wanaodunisha Kiswahili na kuenzi masomo mengine hasa ya Sayansi.
Uwapo wa chama hiki shuleni umeamsha ari ya mapenzi ya Kiswahili miongoni mwa wanachama ambao kwa sasa ni mabalozi halisi wa Kiswahili na wasomaji na wazalendo wakubwa wa gazeti hili la Taifa Leo.