Waititu awataka Wakenya kutoyumbishwa na mihemuko ya wanasiasa
Na LAWRENCE ONGARO
WANANCHI wamehimizwa wasikubali kuyumbishwa na siasa zinazoendelea kwa sasa hapa nchini.
Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, alisema chama cha Jubilee hakitakubali kuyumbishwa na wale aliowataja kuwa ni “wageni waliojiunga nacho hivi majuzi.”
Alitoa mwito kwa Jamii ya Mlima Kenya kuwa makini katika siasa zinazoendelea kwa sasa.
“Sisi kama Jamii ya Mlima Kenya kama tulifanyiwa vizuri na jamii nyingine, kwa nini tuonekane kama watu wasioaminika? Ninasema hivyo kwa sababu hatutaki kujadiliwa kama jamii isiyoaminika siku za usoni,” alisema Bw Waititu mnamo Jumatatu katika eneo la Happy Valley (Landless), mjini Thika, Kaunti ya Kiambu, wakati alikwenda kuzindua mradi wa kuunda bomba la kusukuma maji ya mvua ambayo huwa tishio kwa wakazi wa eneo hilo.
Alisema eneo hilo ni la kilomita mbili na mradi utagharimu Sh50 milioni na unaotarajiwa kukamilika miezi miwili ijayo.
Alisema hata ingawa mambo ya ufisadi unaoendelea kuchunguzwa miongoni mwa viongozi yanaendelea, siasa haiwezi kuingizwa hapo kwa sababu inaweza kuleta taharuki nchini.
Alisema hata ingawa tunazidi kushirikiana na wenzetu wa upinzani, ni sharti tuwe macho tusije tukaachwa kwa ‘mataa’ dakika za mwisho tusijue la kufanya.
Alisema wakazi wa eneo hilo watajengewa kituo cha polisi kwa gharama ya Sh500,000.
“Ninajua hali ya usalama imekuwa mbaya kwa muda mrefu lakini ninaamini mara tu baada ya kujenga kituo hicho, mambo yatakuwa mazuri,” alisema Bw Waititu.
Alisema mpango wa kuunganisha kampuni nane za maji ulikuwa wa busara lakini kampuni moja ya Thiwasco Water Company ilipeleka malalamishi mahakamani kuwa hawataki mpango wa kuwaunganisha na zingine.
Alisema yeye kama gavana wa watu wote Kiambu atafanya kazi kwa kujitolea na bila kujali huyu ni wa kabila hili ama lile.
“Mimi kwa sasa sitaki kujihusisha na siasa duni. Ninataka nifanye kazi yangu kwa uwazi na usawa. Kila mkazi wa Kiambu ni wangu na nina haki ya kumhudumia,” alisema Waititu.
Spika wa bunge la Kaunti ya Kiambu, Bw Stephen Ndichu, alisema malumbano ya viongozi kuhusu maswala ya ufisadi yanatia hofu.
“Ufisadi usiwe kama silaha ya kushambulia wengine. Ni muhimu uchunguzi ufanywe kwa njia ya uwazi na usawa bila kuingiza siasa za chuki,” alisema Bw Ndichu.