Mpango wa serikali kupunguzia wananchi nauli
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI itaanza kukadiria na kusimamia nauli zinazotozwa na magari ya uchukuzi wa umma kote nchini ikiwa bunge litalipitisha marekebisho kwa Sheria ya Trafiki na ile inayosimamia Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA).
Waziri wa Uchukuzi James Macharia aliwaambia wabunge kwamba hatua hiyo inalenga kukinga wananchi dhidi ya kupunjwa na wenye magari hayo kupitia nyongeza za nauli kiholela.
Kwenye taarifa iliyowasilishwa Jumatano kwa niaba yake kwa kamati ya bunge kuhusu uchukuzi na Waziri Msaidizi katika Wizara hiyo Chris Obure, Bw Macharia alisema kuwa wizara yake itawasilisha mapendekezo hayo kwa baraza la mawaziri kabla ya kuwasilishwa bungeni.
Wizara hiyo ya uchukuzi inapendekeza kuifanyia marekebisho sehemu ya 119 (1) ya Sheria ya Trafiki kwa kuanzisha ibara nyingine ambayo itamruhusu Waziri wa Uchukuzi kuamua namna nauli za magari ya uchukuzi yatadhibitiwa.
Marekebisho hayo ya sheria yakipitishwa waziri atakuwa na uwezo wa kisheria wa kubaini mfumo wa kuweka mwongozo kuhusu nauli, mbuni za kubadilisha viwango vya nauli na kuweka adhabu kwa wale ambao wakakiuka mwongozo huo.
Wizara hiyo vile vile inapania kufanyia marekebisho sehemu ya 4(2) ya Sheria ya NTSA kwa kuanzisha ibara mpya itakayotoa nafasi kwa asasi hiyo kuanzisha mwongozo wa nauli ya magari ya uchukuzi.
“Marekebisho hayo ya sheria yataiwezesha NTSA kusimamia nauli sawa na jinsi Tume ya Kawi Nchini inavyosimamia bei ya mafuta,” Bw Macharia akasema.
“Tayari mchakato huo umeanza na unashughulikiwa na maafisa wetu wa idara ya sheria. Mapendekezo yatawasilishwa kwa baraza la mawaziri hivi karibuni kwani maafisa hao wameamriwa kuharakisha kazi hiyo,” Bw Obure akasema alipokuwa akisoma taarifa hiyo mbele ya wabunge kwa niaba ya mkubwa wake.
Waziri huyo msaidizi alisema serikali inafahamu kwamba wananchi hunyanyaswa na magari ya uchukuzi akisema marekebisho hayo ya sheria yanalenga kuwakinga wananchi dhidi ya upunjaji huu.
Sekta ya Uchukuzi wa Umma kusimamiwa na Sheria ya Trafiki Sura ya 403, Sheria ya NTSA Nambari 33 ya mwaka wa 2012 na kanuni husika.
Chini ya sheria hizi, hamna kipengee kinachoiba mamlaka hiyo uwezo wa kusimamia na kubaini nauli zinazotozwa na magari ya uchukuzi wa abiria (PSVs). Hali hii ndio imefungua mwanya kwa wenye magari hayo kuongeza nauli kiholela.
“Pana haja ya kulinda raia dhidi ya unyanyasaji wa PSVs kwa kudhibiti nauli za magari hayo. Chini ya mpango huu, inatarajiwa kuwa NTSA itaweka viwango vya nauli, kwa kubaini viwango ambavyo magari yanapasa kutoza katika kila ruti,” Bw Macharia akaambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing.
Bw Pkosing alisema kuwa mapendekezo hayo ya marekebisho ya sheria yalikuwa yakisubiriwa kwa hamu, akisema kuwa kero la wananchi kutozwa nauli za juu limekithiri kote nchini.
Swali hilo la abiria kutozwa nauli za juu kupita kiasi iliwasilishwa kwa wizara hiyo na Mbunge wa Bomachoge Borabu Zadoc Ogutu ambaye alisema hali hiyo imekuwa ikishuhudiwa katika barabara kadhaa katika kaunti ya Kisii.
Alitoa mfano wa ruti ya Kisii- Mogonga- Magena ambako alisema nauli iliongezwa kwa kiwango cha asilimia 100 baada ya kurejelewa kwa sheria za Michuki mwishoni mwa mwaka jana.
“Natumai kuwa marekebisho haya ya sheria yatapitishwa kusudi wananchi wapate afueni. Mwenendo huu wa kutoza nauli za juu kupita kiasi umekithiri zaidi miongoni mwa matatu, na ni jambo la busara kwetu kuwakinga wananchi dhidi ya unyanyasaji,” akasema Prof Ogutu.
Serikali ilirejesha sheria za Michuki mwishoni mwa mwaka jana ili kurejesha nidhamu katika sekta hiyo ya uchukuzi wa umma kufuatia ongezeko la visa vya ajali ya barabarani.
Lakini wenye magari walitumia nafasi hiyo ya kuongeza nauli kupita kiasi hali iliyopelekea wananchi kulalamika. Wakazi wa Nairobi pia hukumbwa na kero hili nyakati za msongamano au mvua inapoanza kunyesha ghafla.