Habari

Mgawanyiko katika Jubilee

March 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

UBASHIRI wa maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Samson Cherargei (Nandi) mwaka 2018 kuwa muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga ungevunja Jubilee, sasa umeonekana kutimia kufuatia migawanyiko inayoshuhudiwa ndani ya chama hicho.

“Ikifanana na mbata, ikitembea kama mbata na kuwika kama mbata, ni mbata. Bw Odinga anatuambia muafaka ni wa kuunganisha nchi, ilhali washirika wake wa kisiasa wanaongea kuhusu 2022. Hii inamaanisha hana nia nzuri katika suala hili,” alisema Bw Murkomen wakati huo.
Naye Bw Cherargei alisema: “Tunajua Raila amezoea kubomoa vyama lakini wakati huu hatutakubali.”
Mwaka mmoja baadaye, Jubilee sasa imegawanyika katika kambi mbili kuu, moja ikimuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na nyingine Naibu Rais William Ruto.

Makundi hayo mawili yamekuwa yakilumbana vikali, ishara kwamba huenda ikawa vigumu kuzima moto unaoteketeza nyumba ya Jubilee.

Mgawanyiko ndani ya Jubilee ulianza kujitokeza mara baada ya mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, wakati baadhi ya wanasiasa walipotilia shaka nia ya kiongozi huyo wa ODM hasa alipotuliza siasa kali ghafla, mwezi mmoja tu baada ya kuweka taifa kwenye taharuki kufuatia kiapo cha kuwa ‘rais wa wananchi’.

Wanasiasa hasa wa kambi ya Dkt Ruto, walikaribisha mwafaka huo kwa tahadhari na wameendelea hivyo hadi sasa, wakisema rekodi ya Bw Odinga katika maafikiano ya kisiasa ni ya mtu asiyeweka maagano. Hii ni kufuatia Bw Odinga kusambaratisha Kanu, kuondoka Narc, kuhama Cord na hatimaye NASA.

Vita dhidi ya ufisadi

Mbali na ‘handisheki’, mfarakano wa Jubilee pia umechochewa na vita dhidi ya ufisadi, siasa za urithi wa 2022 na mjadala kuhusu kura ya maamuzi.

“Masuala hayo manne ndiyo yanayomaliza Jubilee. Kufikia mwisho wa mwaka huu, chama hicho kitakuwa kimepasuka vipande vipande,” asema mbunge mmoja kutoka Mlima Kenya wa kambi ya Dkt Ruto.

“Nina hakika kuna mipango ya watu wanaotaka kutimiza malengo yao ya kibinafsi kuvunja Jubilee. Lakini kiini kikubwa ni muafaka ambao kwa kila hali umemtenga Naibu Rais serikalini,” alisema mbunge huyo ambaye aliomba tusitaje jina lake.
Wandani wa Dkt Ruto hasa kutoka eneo la Rift Valley, wanadai kwamba handisheki imevuruga mpangilio uliokuwepo wa chama cha Jubilee kuhusu 2022.

Wanasiasa walio msitari wa mbele kukosoa ‘handisheki’ ni maseneta Murkomen, Cherargei na Aaron Cheruiyot wa Kericho. Wengine ni wabunge Caleb Kositany wa Soy, Oscar Sudi wa Kapsaret na Gavana wa Nandi Stephen Sang.

Mara kwa mara, Dkt Ruto mwenyewe amekuwa akikosoa ‘handisheki’ akisema hailengi kuunganisha Wakenya bali kumtimua kutoka chama cha Jubilee.

“Hatutakubali mlete utapeli serikalini na kuvunja chama cha Jubilee, hili hatutakubali,” Bw Ruto amenukuliwa akisema mara kadhaa.

Kulingana na Seneta Murkomen, mjadala kuhusu kura ya maamuzi na vita dhidi ya ufisadi vinalenga azma ya Dkt Ruto ya kugombea urais.

“Nia ni kuleta mkanganyiko katika chama cha Jubilee ili mpangilio uliokuwepo awali usitimie,” Bw Murkomen amekuwa akisisitiza.

Waondoke Jubilee

Japo amejitenga na siasa, Rais Kenyatta alishangaza wengi kwa kuwaambia wakazi wa eneo la Mlima Kenyatta kwamba watashangaa atakapoteua mrithi wake.

“Hakujakuwa na mkutano wa kamati kuu ya chama au wabunge wa chama tangu ‘handisheki’,” alilalama Bw Cheruiyot majuzi.

Wabunge wa Jubilee wanaomuunga mkono Rais Kenyatta katika vita dhidi ya ufisadi nao wanamshinikiza Dkt Ruto na wandani wake kujiondoa serikalini badala ya kulalamika.

“Kama wanataka kuondoka serikalini waende bila kupiga kelele,” alisema mbunge wa kuteuliwa, Maina Kamanda.

“Hakuna mahali palipoandikwa kwamba ni lazima Ruto awe rais,” alinukuliwa Mbunge wa Nyeri Mjini, Ngunjiri Wambugu.

Kulingana na mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, Jubilee kimekufa na ni vigumu kukifufua, akiongeza kuwa eneo la Mlima Kenya limeanza kutafuta chama cha kutumia kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.