DOMO KAYA: Riri anabisha, nani atamlaki?
Na THOMAS MATIKO
SIJUI kama umezisikia hizi habari kwamba menejimenti ya msanii staa kutoka Marekani, Rihanna inamsaka promota mwenye uwezo wa kumleta Kenya?
Ndio Rihanna.
Kabisa mtoto wa watu kaonyesha nia ya kutaka kuja kuwakosha huku na mambo yake.
Si wajua tena, kando na kuwa na muziki mzuri, mtoto wa watu anapenda kuonyesha sana mwili wake na hasa alivyo mrembo, mrefu wa kimo, we acha tu! Bonge la toto hodari. Wanaume mpoo?
Hizi habari mimi nimezisikia na zikanifurahisa sana. Naweza kutamani kuiona shoo ya laivu ya Rihanna hata kwa dakika 10 tu, itatosha.
Nipo radhi kulipia tiketi hata kama itanigharimu Sh25,000 VVIP japo kumwona laivu akifanya yake.
Nina uhakika sipo pekee yangu katika mawazo haya.
Na kwa anayeniona kama vile nimepagawa, basi labda nikukumbushe tu mwaka jana wenzako walilipia tiketi za VVIP Sh15,000 kumwona Mondi kwenye Wasafi Festival. Sasa nini tena?
Taarifa za Rihanna kuja huku ziliibuliwa na promota Mike Strano aliyesema kwamba amepokea barua kutoka kwa menejimenti ya staa huyo ikiwa inamsaka promota mwenye uwezo wa kufanikisha shoo Afrika Mashariki kati ya Septemba na Oktoba.
Hapa promota anayehitajika ni mtu asiyebabaishwa na hela pengine bilionea hivi. Naye awe na uhakika kwamba atajaza ukumbi wowote ule kwa namna Wakenya wanavyopenda sherehe halafu hii itakuwa inamhusu Rihanna.
Ninajua baadhi yenu mtakuwa mnawaza, kama waliweza kumleta Chris Brown na akalipwa Sh90 milioni kwa shoo ya saa nzima iweje wasiweze kumleta Rihanna.
Ni mwanadada
Bwana eeeh! Rihanna ni habari nyingine kabisa. Ndio ni staa wa hadhi ya Breezy lakini pia huyu ni mwanadada ujue.
Kisha Rihanna anavyojipanga kwenye ziara zake ni taabu. Breezy alipokuja, aliongozana na mabaunsa wake, meneja na mpiga picha basi.
Rihanna mzee unaambiwa anasafiri na timu ya watu 60. Yaani anakusanya kijiji kidogo kama cha kule kwetu Komotobo, Kuria.
Kijiji cha Rihanna kila mtu ana kazi yake maaalum, kuanzia kwa wapambaji wake, wabunifu mavazi, yaani wewe acha tu.
Hawa wote lazima walipiwe nauli ya ndege na pia vyumba 20 kwenye hoteli za 5 Star kwa mujibu wa menejimenti yake.
Bado hujaweka hesabu ya usafiri na msosi. Umeona kwa nini hizi ni hesabu za kibilionea ndizo zinazohitajika hapa?
Najua Kenya watu wana hela, kwa nchi ya wezi kama hii, watakosaje? Licha ya yote bado hajapatikana promota anayejiamini. Ila akilini mwangu nawaza, kama waliweza kumleta Breezy, tamasha ambayo tetesi zinadai kuwa Sultan Hassan Ali Joho naye alichangia kufanikisha, mbona na hili asijaribu sababu najua naye anapenda sherehe kwelikweli.
Au mbona Safaricom wasiizamie fursa hii? Kama Jazz wamefanikisha miaka yote hiyo, Rihanna mwenye uhakika wa kuwaletea faida watashindwa?