Sky-Life Karate Club Nakuru wavuma
Na LAWRENCE ONGARO
KLABU ya Karate ya Sky-Life Karate Club imeibuka kuwa tisho katika mji wa Nakuru ikiwa na vijana chipukizi.
Kocha wake Michael Obura anasema amekuwa na klabu hiyo kwa zaidi ya miaka kumi na ameweza kuwanoa vijana wengi.
“Kwa kweli mchezo wa karate ni wa kipekee kwa sababu humfanya mchezaji kuwa na nidhamu ya hali ya juu. Mchezo huo unahitaji unyenyekevu na utiifu wa hali ya juu,” asema Obura.
Alisema kikosi chake kina wanakarate wapatao 40, lakini kulingana naye, mchezaji anayehudhuria mazoezi kila mara ndiye hupata nafasi ya kucheza.
“Mimi sibagui mchezaji yeyote. Langu ni kuona kila mmoja akijisikia anathaminiwa. Kwa hivyo, kila mwanakarate sharti ajitume mazoezini,” asema kocha huyu.
Anasema alijiunga na karate akiwa na umri wa miaka minane pekee na tangu wakati huo hadi sasa amecheza kwa miaka 23.
“Mimi kwa upande wangu nina ujuzi wa kutosha na ndiyo maana niliwazia kuwakuza vijana chipukizi mjini Nakuru,” anasema.
Waonyesha umahiri
Hivi majuzi katika mashindano ya Karate Opens Championship katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya, Thika, timu ya Sky-Life Karate Club ilikuwa na wachezaji 11 ambao walifika kuonyesha umahiri wao.
Wachezaji hao walikuwa kati ya miaka 6 hadi 23 ambao wengi waliweza kuibuka na medalist ya dhahabu na fedha.
Mchezaji Peter Mandiri, 17, alishinda dhahabu katika mchezo wa Kata na ule wa Kumite.
Mwanadada Selina Atieno, 19, alizoa dhahabu katika mchezo wa Kata.
Lydia Muthoni, 12, alipata dhahabu na fedha katika Kata na Kumite mtawalia.
Naye King Mburu, 12, alipata nishani mbili za fedha katika mchezo wa Kata na Kumite.
Naye Morgan Otieno mwenye umri wa miaka 12 alijishindia nishani mbili za fedha katika Kata na Kumite.
Kocha Obura anasema kikosi hicho hufanyia mazoezi katika shule ya upili ya Flamingo mjini Nakuru siku za Jumatatu, Jumatano, na Ijumaa kutoka saa kumi na moja na nusu jioni hadi saa mbili za usiku.
Maafisa wengine wanaoendesha kikosi hicho ni mwenyekiti Denis Sasati, halafu katibu ambaye anashikilia wadhifa wa mwekahazina na ambaye ni Tabitha Ndung’u.