MWANAMUME KAMILI: Mfujaji jasho lake hana budi kujiandaa kwa dhiki uzeeni
Na DKT CHARLES OBENE
LABDA umewahi kuwaona wazee wa makamo wanaolala kwenye milango ya maduka ama kwenye stani ya mabasi ukajiuliza walikotoka!
Jongea nikujuze asili ya babu na bibi waliokatalia mijini badala ya kwenda mashambani kucheza na wajukuu!
Mwisho wa upumbavu ni fadhaa na dhiki isiyomithilika!
Taabu wanazopitia wakongwe hawa mijini ni msiba wa kujitakia. Hawastahili pole! Mwanamume mfujaji wa jasho lake hana budi kujiandaa kwa dhiki uzeeni.
Hatima ya ufasiki na ubugiaji vileo ni kulala milangoni ama maegeshoni.
Kuna misiba ambayo humfika mwanadamu naye akashindwa kabisa kujieleza au kutathmini vipi msiba ule kamfika!
Mwanadamu anaweza kujitahidi kwa udi na uvumba kuyapanga yake lakini mwisho wa siku mapenzi ya Mungu hutimia.
Hebu tulizeni uchu nyie mnaowashwa kukatia kamba pembamba. Kauli hii haimaanishi kwamba wanadamu wacheze pute tu ama wajikokote kutoka kitandani mwendo wa adhuhuri kuelekea jikoni.
Ili kubadili mkondo wa maisha, wanadamu hasa wanaume wa leo wanastahili kuhakiki hali zote na kuchagua maamuzi mema.
Ninasisitiza umuhimu wa maamuzi mema kwa kuwa ndio mwanzo wa mambo kunyooka.
Gumegume
Wengi wa kina yakhe wanaotapatapa na kuranda mitaani ndio kwanza wanagundua umuhimu wa kuchagua mema badala ya kufuata upepo jinsi wanavyofanya gumegume wa leo.
Kuna baadhi ya wafanyakazi waliofika kustaafu ila hakuna cha thamani kinachoashiria kwamba walikuwa kazini kwa miaka na mikaka! Yaani hawana mbele wala nyuma.
Hawana kuta wala msingi wa kiota sisemi nyumba ya binadamu. Jamani nielezeni mdudu mwenye mazoea kufukarisha wanaume wa leo? Mahambe hawa ndio kwanza wanasubiri jumuia kuwachangia fedha angalau kuwaondelea fedheha na kuwapa jeneza na sanda.
Kitovu cha matatizo ya baadhi ya wanaume wa leo ni mbegu ya maamuzi mbovu walizofanya siku za shingo kuongoza kichwa.
Badala ya kula kidogo na kuweka akiba, gumegume hawa walikula mbegu na mbolea vilevile. Walianza kunywa ujira na marupurupu kabla kunywa mikopo yote waliyopokezwa na benki.
Na sio kunywa tu, wazee hawa walianza kuoa himaya ya wanawake na kuolewa wangali vijana.
Isitoshe, wanaume walijipa shughuli za kutunza wajane na watoto wao. Wakawa ndio wafadhili wa miradi ya maendeleo iliyolenga kuwapumbaza wajane na jamii zao.
Vipi mwanamume mwenye akili timamu anaweza kuasi kwake mashambani akasalia jijini kunywa mchuzi uliochemshwa kutoka vichwa vya mbuzi na kondoo?
Mtu hula jasho lake! Ndivyo wanavyosema wangwana wa leo. Lakini katika ulaji wa jasho inabidi mwanamume kukumbuka kwamba ipo siku jasho litakaukia pajini mja akasalia kumeza mate mfano wa shubiri.
Unywaji kupindukia pamoja na ufasiki wa wanaume wa leo umechangia pakubwa kuwepo wazee waliostaafu lakini wakashindwa jinsi ya kwenda mashambani.
Awali, wanawake ndio waliohamia kwenye viota vya wanaume. Leo mambo ni kangaja! Imekuwa desturi wakongwe wa leo kuhamia nyumba za wajane ambao wenyewe wanategemea wahisani tu.
Sijamwona mbuzi kajipeleka kwenye chaka la fisi akarudi mbuzi! Mwanamume mwenye akili ya zege anaweza geuzwa zeze; nyaya kuchunwa tu kwa raha za wacheza ngoma! Baadhi ya wazee wanaolala kwenye stani za mabasi wamefukuzwa kutoka nyumba za wajane walikohamia siku za awali walipokuwa watu wa vyao.
Ndiyo sasa wazee hawa wanagundua ukweli wa mambo kwamba mwenye shombo hana kutuzi ilmuradi kipochi kimejaa pomoni!
Wajibu wa vijana wa leo ni kutafuta babu, baba na bibi waliokatalia mijini na kuwapeleka moja kwa moja hadi mashambani.
Isitoshe, wajifunze kutoka dhiki zao angalau wasijerudia makosa ya kula mishahara na kuzifuja pesa katika anasa na starehe!
Hawa vijana wanaokesha kwenye rununu badala ya kudurusu masomoni ndio kwanza wanapanda mbegu mbaya.
Vipi binadamu mwenye akili timamu kukataa kuimarisha maisha masomoni na badala yake kukesha kujipumbaza kutazama picha za uchi ama kanda za video zisizoweza kubadili maisha ya mtu!
Lau mngalijua dhiki wanazopitia babu, baba na bibi hawa kwenye mitaa ya miji, mngaliwajibika masomoni. Natamani sana watoto wenu kufukuzwa shule kwa ukosefu wa karo.
Angalau mtakumbuka kwamba mlicheza densi kwenya mabaa badala ya kuchezesha ubongo maktabani. Ndipo mtajutia uvutaji bangi badala ya unywaji kahawa.
Afadhali wangu dawa yake kahawa tu! Thamani yake siwezi mithilisha na chochote duniani. Mke mwema yule. Kaongoka mwanamtu! Ole nyinyi mliovumbua unywaji pombe badala ya sharubati vyuoni! Ujinga wa ujanani ni gharama uzeeni.