Michezo

Kenya yavuna medali za dhahabu mashindano ya Olimpiki kwa wenye ulemavu UAE

March 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imezoa medali mbili za dhahabu Jumamosi katika mashindano ya Olimpiki kwa watu wenye ulemavu yanayoendelea jijini Abu Dhabi katika Milki za Kiarabu.  

Medali ya kwanza ilipatikana katika fani ya bocce pale Wakenya Deepak Sanghvi, Effie Owuor, Marion Iravaya Obiri na Veer Rajesh walizoa dhahabu.

Fani ya bocce ina Wakenya Deepak Sanghvi, Effie Owuor, Marion Iravaya Obiri na Veer Rajesh na walizoa dhahabu. Picha/ Hisani

Timu hii ya Wakenya ilikamilisha mbele ya Mauritius, Oman, Romania na Chinese Taipei zilizofuatana kutoka nafasi ya pili katika usanjari huo.

Naye Onesmus Mutinda alishindia Kenya taji la Half Marathon.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 20 alikamilisha mbio hizi za kilomita 21 kwa saa moja, dakika 11 na sekunde 34.

Onesmus Mutinda alishindia Kenya taji la Half Marathon. Picha/ Hisani

Alikamilisha dakika 14 mbele ya mpinzani wake wa karibu Anwer Elmabrouk Ali Dakam.

Dakam, 33, kutoka Libya alitimka kwa saa 1:25:27 naye Nikolaj Hjalmar Vomb Mortensen, 23, kutoka Denmark akafunga mduara wa tatu-bora kwa saa 1:25:43.

Waogeleaji Faith Muchiri, Charlton Waithaka, Sonali Ritesh na Kagondu Kariuki wamenyakua nishani ya fedha katika kitengo cha 4×25 relay.

Kenya inawakilishwa na wanamichezo 71.

Inashiriki soka, mpira wa vikapu, voliboli, voliboli ya ufukweni, handiboli, riadha,bocce, kuendesha baiskeli, gofu, kuogelea kwenye bwawa na kuogelea katika mto, ziwa ama bahari (Open Water Swimming).

Mashiondano haya ya dunia yalianza rasmi Machi 14 yakihusisha zaidi ya mataifa 170. Yatakamilika Machi 21.