• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Agora wasanii wenye azma ya kufikia upeo wa Wasafi Classic Baby

Agora wasanii wenye azma ya kufikia upeo wa Wasafi Classic Baby

NA RICHARD MAOSI

UKITAKA kung’amua urojo wa ngoma, basi mwenyewe ingia ndani ucheze. Hii ndiyo kaulimbiu ya kundi la Agora Music School, wanamuziki shupavu kutoka Kaunti ya Nakuru.

Wakiwa watumbuizaji, wachoraji, malenga na waimbaji stadi, sanaa ya kupiga ala za muziki ndiyo inawatofautisha na makundi mengine ya burudani nchini Kenya.

Makali yao jukwaani yakionekana kufanikisha sherehe za kitaifa uwanjani Afraha, ikiwemo Siku ya Mashujaa, Madaraka, Leba Dei miongoni mwa hafla nyinginezo zenye hadhi.

Viongozi wa kaunti wamekuwa wakitumia huduma zao kuwasisimua wageni wanaofika Nakuru, hususan kutalii kutoka ukanda wa jumuia ya Afrika Mashariki.

Mercy Wairimu mwanafunzi wa muziki na mashairi akijipiga msasa kabla ya kushiriki kwenye tamasha. Picha/ Richard Maosi

Agora wameibukia kufuata nyayo za aliyekuwa msanii nguli ya Pop kutoka Marekani Michael Jackson, wakisema alikuwa na ufuasi mkubwa kwa kuteka hisia za hadhira.

Bali na kujijengea jina, wamehusika katika shughuli za kutangaza bidhaa kama vile mafuta ya kujipaka, taasisi za elimu na huduma za simu kwa wateja.

Mashabiki wao ni vijana na wazee, wa kila umri na rika kutoka ndani na nje ya Kaunti ya Nakuru.

Mjini Nakuru wao huendesha matamasha yao eneo la Milimani, Menengai Social Hall , Nakuru Athletics Club na wakati mwingine kuitikia mialiko rasmi ya vyuo na shule za upili.

Agora wameweka mikakati ya kufanya kolabo na wasanii mahiri kama vile Khaligraph Jones na King Kaka ili kupanua wigo na kuongeza idadi ya mashabiki.

Ngomo hupigwa ustadi wa aina yake ili kuoana na gitaa na sauti za ala nyingine. . Picha/ Richard Maosi

Kufikia sasa wamerekodi vibao kama vile, You Are Faithful na kucheza filamu ya Cheers chini ya mwavuli wa Agora Records kati ya mwaka wa 2016 hadi 2018.

Kibao cha You Are Faithful kilifanya vizuri katika chati za redio mitaani, Agora wakionekana kuwafunika wasanii watajika kwa kushikilia nambari moja kwa wiki 10 mfululizo.

Wakati mwingi wanaimba nyimbo za injili, kwa sababu wametilia maanani swala la maadili wakiamini muziki wao utapenya na kuwafikia watu wa kila rika.

Mwasisi wa Agora George Oula, alieleza Taifa Leo Dijitali kwamba hana budi kushirikiana na vijana ili kuwatoa kwenye lindi la umaskini kwa kutumia vipaji vyao ipasavyo.

Mkali wa gitaa atabasamu baada ya kuhojiwa na Taifa Leo Dijitali. Picha/ Richard Maosi

“Kionekanacho kikubwa huanza kwa hatua moja kabla ya kufikia mbali na bila shaka vijana hawa wameonyesha wana nia ya kuchangia,katika hazina ya talanta,” alisema.

Anaungama kwamba wasanii wa kizazi kipya hupitia changamoto nyingi kabla ya kukomaa na safari, wengi wao wakipoteza mwelekeo njiani na kugeukia maisha ya starehe na anasa.

Janga la kutumia mihadarati pamoja na shinikizo la kutafuta umaarufu, baada ya muda mfupi likiwaponza kwa asilimia kubwa.

“Wasanii wanahitaji kuwa kioo cha jamii, wawe na uwezo wa kubuni kazi zinazoangazia hali halisi ya mtu wa kawaida,” alisema.

Usipige tu gitaa, tazama kama wacheza densi wanafuata mapigo yako wanaponengua viuno. Picha/ Richard Maosi

Baadhi ya wanamuziki wa Bendi ya Agora tuliozungumza nao ni pamoja na Nelly Mwangi na Dominic Ouma.

Kwa miaka mitatu wamekuwa wakicheza ala za muziki na kujifundisha ustadi wa kunengua viuno kwa kuzingatia mitindo ya kisasa.

“Kazi zetu nyingi humulika siasa, bidii na kazi, nafasi ya mwanamke katika jamii, umaskini, elimu, taasubi za kiume na utunzaji wa mazingira,” Domonic alisema.

Agora imekuwa ikitoa hamasisho kwa vijana, na kuwawezesha kurekodi vibao mbali na kuwatafutia soko burudani kimataifa, kupitia mtandao wao wa kijamii (Agora School).

Wasanii wa Agora wakifanya mazoezikabla ya kushiriki tamasha la muziki mjini Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Mmoja wao ni David Juma almaarufu kama Sparkly Majuu kutoka nchi jirani ya Tanzania,lakini sasa anaishi mjini Eldoret.

Majuu ametamba na vibao zaidi ya 20 chini ya lebo kali ya Two Touch eneo la Mlolongo, Kaunti ya Machakos.

Amerekodi kibao Hivyo hivyo, Mrembo, Ni Wewe, Nisamehe, Nyota, Maisha ya Kitaa miongoni mwa vingine.

Produsa wake Tony Touch humfanyia kazi ya kutengeneza mawimbi ya sauti na kuleta ladha tofauti ya muziki Afrika Mashariki.

Hivi karibuni atazuka na kazi mpya akiwa ameshirikiana na Nay wa Mitego na Timbula katika mradi anaoamini utatetemesha chati za vibao vya Bongo.

Msanii Sparkly Majuu kutoka Bongo aliyefaidika na mradi wa Agora tangu aanze kushirikiana nao. Picha/ Richard Maosi

Safari ndefu ya Agora katika uwanja wa burudani ilianza mnamo 2015 George Oula alipobaini amejaliwa kipaji cha kuimba mbali na kucheza gita.

Kwa ushirikiano na rafiki zake kutoka mtaani London, Nakuru walibuni lebo ya kurekodi nyimbo za injili.

Lebo yenyewe haikudumu muda mrefu, kikosi kilipovunjika kisha akaanza binafsi kwa kutafuta wahisani.

Ni wakati huo wazo la kuazisha shule ya kufundisha muziki ilimjia, akajitahidi kuweka mikakati, kabla ya na akaendelea kujiboresha.

Muziki huanza kwa roho, kabla ya kupandishwa kwa akili kisha kutokea kwenye kinywa. Picha/ Richard Maosi

George amefanikiwa kuona mengi, licha ya wanamuziki kadhaa kupitia mikononi mwake, akiamini kwamba kipaji kinalipa.

Ametangamana na watu wengi, wenye hadhi mbalimbali serikalini kutokana na kipaji chake katika ulingo wa sanaa ya muziki.

Bali na kunyanyua mataji mengi ametambulika katika hafla kwa heshima, akitajwa kama balozi wa muziki wa kizazi kipya.

George alitambuliwa 2017 na serikali ya Kaunti ya Nakuru, Idara ya Vijana na Michezo kama mwandishi wa mashairi tajika anayekuja kwa kasi.

Kila msaii katika kundi hili ana ari ya kujua kucheza kila aina ya ala za muziki. Picha/ Richard Maosi

Familia ya Agora inamtambua kama mtungaji na mwandishi wa mashairi kwa hafla kwa mujibu wa maswala yanayozunguka jamii.

Mmoja wa wasanii hapa,Nelly Mwangi anasema ni wajibu wa msanii kusikiliza mawazo ya umma kabla ya kutoa kibao.

“Kama njia ya kusawazisha tamaduni mbalimbali duniani, kuenda na wakati na kukubali mabadiliko ni mambo mawili yasiyoweza kutengana,” alisema.

Hili linajiri siku chache baada ya mkurugenzi wa Bodi ya Filamu na Muziki nchini Dkt Ezekiel Mutua kupiga marufuku baadhi ya vibao.

Kazi njema bila shaka hutuzwa. Usishangae kuona matunda mazuri katika mzabibu uliopaliliwa vizuri. Picha/ Richard Maosi

Bodi ya MCSK imeweka masharti makali kwa wachezaji filamu na waimbaji ikiwataka wazingatie maadili katika kazi zao.

Dkt Mutua anafahamika kwa kuzuia kibao cha Kwangaru, chake wasanii Diamond Platnumz na Harmonize kutoka Tanzania na kingine cha Sauti Sol.

Lakini kundi la Agora linafuata sheria na maadili ya kijamii linapotunga mashairi na nyimbo zake, huku likijiepusha na kuingiliwa na mienendo ya utamaduni wa mataifa yaliyoendelea ambayo hutunga na kurekodi video za ngono kwenye nyimbo.

Ndoto yao ni kutoa vibao vinavyotetemesha Afrika zima jinsi wafanyavyo wasanii wa Wasafi Classic Baby (WCB) wa Tanzania ambao wengi wanakiri kuwa ni manguli wa utunzi na uimbaji.

 

You can share this post!

Murkomen amtaka Uhuru ampige kalamu Kinoti

Mijadala ya ufisadi yafunika njaa inayotafuna maelfu ya...

adminleo