AP aliyedaiwa kuua mwalimu anaswa akivuka mpaka
Na SHABAN MAKOKHA
AFISA wa polisi aliyekuwa akisakwa kwa kushukiwa kumuua mwalimu wa shule ya upili ya Navakholo, Kaunti ya Kakamega alikamatwa Jumamosi akijaribu kuvuka mpaka kuingia Uganda saa chache baada ya wakazi kutisha kutumia uchawi kumwadhibu.
Mkuu wa polisi eneo la Magharibi, Rashid Yakubu, alithibitisha kuwa Patrick Nyapara alikamatwa na atachukuliwa hatua za kisheria.
Wakazi wa Navakholo walikuwa wameshinikiza akamatwe au wazee watumie nguvu za kitamaduni kumrudisha na kumwadhibu kwa kutafuna nyasi sokoni.
Walidai kwamba huenda polisi walikuwa wakimlinda afisa mwenzao kwa kukosa kumkamata ashtakiwe.
Wakiwa na hasira, wakazi walikusanyika katika soko la Navakholo kufuatia kuuawa kwa Christine Maonga, aliyekuwa mwalimu katika shule ya upili ya Navakholo. Afisa huyo alitoroka baada ya kumuua mwalimu huyo Alhamisi.
Kwenye mkutano ulioitishwa na mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe na ulihudhuriwa na Naibu Kamishna Geofrey Tanui na mkuu wa polisi Jacob Chelimo wakazi walitisha kutumia za jamii yao kumkamata. Mkazi Jacob Sifuna, aliwahimiza wazee kuchukua jukumu la kuhakikisha haki imetendeka.
“Tunatoa wito kwa wazee wetu kutumia nguvu zao za kitamaduni ili afisa huyo ajitokeze mwenyewe na kukamatwa. Tunajua na tunaamini wanaweza,” alisema Bw Sifuna.
Kauli yake iliungwa na Bw Emmanuel Wangwe aliyesema wazee wanafaa kutumia nguvu za uchawi ili afisa huyo arudi na kuanza kutafuna nyasi sokoni.
Bw Nyapara alikuwa amehudumu eneo la Navakholo kwa miaka saba. Akiwa katika kambi ya Kaunda, inasemekana alijaribu kumpiga risasi mkazi kabla ya kuhamishiwa Navakholo. Ripoti zilisema alikuwa amemuonya mkewe kwamba angemuua na hata kuandika katika ukurasa wake wa Facebook.
Jana familia ya marehemu ilisema afisa huyo anafaa kukamatwa. Kakake, Bw Kelvin Wesisi, alisema familia ina huzuni kufuatia mauaji ya dada yao miaka mitatu baada ya kuajiriwa.
Baba ya marehemu Fredrick Okumu, alikanusha habari kwamba binti yake alikuwa ameolewa na afisa huyo.