Makala

WASONGA: Tujikakamue kama nchi kumaliza aibu ya raia kufa njaa

March 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI inacheza sarakasi na suala tata la baa la njaa ambalo ni fedheha kubwa kwa taifa hili. Inasikitika kuwa wananchi wameripotiwa kufa kwa njaa maeneo kadhaa nchini ilhali serikali ilifahamu fika kuwa kiangazi hushuhudiwa kila mwaka kutokana na mabadiliko ya hali ya anga.

Nasema serikali inacheza sarakasi na tatizo hilo kwa sababu inafahamu fika kwamba njaa ni zao la usimamizi mbaya wa sekta ya kilimo. Mfano hapa ni usimamizi mbaya wa mradi wa unyunyiziaji maji wa shamba kuu la Galana –Kulalu ambao licha ya kufyonza Sh17 bilioni, haukuzalisha magunia 40 milioni ya mahindi ilivyokadiriwa.

Ni aibu kwamba serikali, kupitia Wizara ya Ugatuzi sasa inatangaza kuwa inasaka Sh8 bilioni za kukabiliana na kero la njaa linaloathiri raia katika zaidi ya kaunti 23 ilhali imekuwa ikijivuta kununua mahindi kutoka kwa wakulima.

Isitoshe, mapema mwaka huu, ilibidi wakulima kutoka maeneo kunakokuzwa mahindi kwa wingi (haswa North Rift) kuandamana barabarani kuishinikiza serikali iwalipe jumla ya Sh3.5 bilioni za mahindi waliowasilisha kwa Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) mwaka jana.

Sasa swali langu ni, serikali itapata wapi Sh8 bilioni inazohitaji kukabiliana na kero hilo ilhali ilichukua muda mrefu kupata Sh3.5 bilioni za kuwalipa wakulima?

Nahofia kuwa itachukua muda mrefu zaidi kwa serikali kupata pesa hizo za kutanzua kero la njaa wakati huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa kufikia Ijumaa, watu saba walikuwa wamefariki kwa kukosa chakula katika eneo bunge la Tiaty, kaunti ya Baringo.

Ili kuzuia athari za kiangazi hiki haraka, serikali inafaa kuandaa bajeti ya ziada na kutenga Sh8 bilioni humo. Kisha bajeti hiyo iwasilishwe bungeni wiki hii ili wabunge waijadili na kupitisha upesi. Kisha pesa hizo zitumiwe kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa North Rift kwa bei waliopendekeza ya Sh3,600 kwa gunia moja la kilo 90.

Kwa njia hiyo, Wizara ya Ugatuzi inayoongozwa na Waziri Eugene Wamalwa itapata mahindi ya kutosha ya kusambaza katika kaunti za Turkana, Baringo, Isiolo , Samburu na mengiyo ambayo yameathirika. Magunia 7,000 ambayo Bw Wamalwa alisambaza katika kaunti ya Turkana wiki jana ni sawa na tone katika bahari; hayatoshi!

Lakini muhimu zaidi ni uimarishwaji wa kilimo cha unyunyiziaji ambacho hakitegemei mvua. Baa la njaa ni tishio kubwa kwa usalama wa wananchi hata kuliko mavamizi ya magaidi kutoka Somalia.