Makala

JAMVI: Pendekezo vyama vya kisiasa viteue makamishna wa IEBC lashika kasi

March 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), watakuwa wakiteuliwa na vyama vya kisiasa iwapo mapendekezo yaliyowasilishwa bungeni na ambayo yanaendelea kuandaliwa yatapitishwa.

Kuna maafikiano kutoka mirengo yote ya kisiasa kwamba vyama vya kisiasa vinavyowakilishwa bungeni vinafaa kuteua makamishna wa tume ya uchaguzi ili kuimarisha uwazi katika tume hiyo.

“Ni wazi kuwa tume ya sasa haitasimamia uchaguzi mkuu ujao ikizingatiwa kwamba imelaumiwa mno kwa kuvuruga uchaguzi uliopita na pia mizozo ya ndani kwa ndani na madai ya wizi wa pesa,” alisema mdadisi wa masuala ya kisiasa Bonface Waswa.

Muungano wa NASA ulisusia marudio ya uchaguzi wa Agosti 7, 2017 ikidai haingepata haki ukisimamiwa na tume ya sasa inayoongozwa na Wafula Chebukati.

Inasemekana kuwa bunge linaunga mkono mfumo maarufu wa vyama vya kisiasa kuhusika kuteua watakaohudumu katika tume ya uchaguzi ilivyokuwa 1997. Katika mfumo huo uliojulikana kama Inter-Parties Parliamentary Group (IPPG), mashirika ya kijamii pia yalishirikishwa kwa kuteua wawakilishi katika tume.

Wadadisi wanasema japo hatua hii haiwezi kukomesha wizi wa kura kabisa, inaweza kujenga imani katika tume hiyo na uchaguzi kwa jumla kwa sababu vyama vitakuwa vimewakilishwa.

“Ikiwa lengo litakuwa ni kuzuia wizi wa kura, haitawezekana kwa sababu hata 1997 uchaguzi uliposimamiwa na IPPG kulikuwa na madai kwamba Daniel Moi wa chama cha Kanu aliiba kura,” alisema Bw Waswa.

Kufikia sasa, pendekezo hilo limeungwa mara mbili; moja na kamati ya bunge kuhusu sheria (JLAC) inayoongozwa na mbunge wa Baringo Kaskazini William Cheptumo na la pili lililowasilishwa na mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma.

Katika mapendekezo yao, ni wazi kuwa IEBC inahitaji kufanyiwa mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Kamati ya Bw Cheptumo inakubaliana na Bw Kaluma wa chama cha ODM kwamba vyama vya kisiasa vinafaa kushirikishwa katika tume ya uchaguzi kwa kuteua makamishna na mfumo wa IPPG ndio unafaa zaidi. Kulingana na mbunge wa Kandara, Alice Wahome, ambaye ni mwanachama wa JLAC, matatizo yanayokumba Kenya yanatokana na kutohusishwa kikamilifu kwa vyama vya kisiasa katika masuala ya uchaguzi.

“IPPG ilifanya vyema na inatoa usawazishaji tunaohitaji,” alisema akirejelea kamati iliyosimamia uchaguzi wa 1997.

Kulingana na JLAC, IEBC inafaa kuwa na makamishna wanne kutoka vyama vya kisiasa, wanawake wawili na wanaume wawili watakaoteuliwa na Tume ya Huduma ya Bunge. Kamati inaamini kwamba hatua hii itapatia vyama vya kisiasa idadi kubwa ya makamishna saba wa tume ya uchaguzi.

Kamati hiyo inapendekeza kuwa tume za walimu, utumishi wa umma na maadili na kukabiliana na ufisadi zinafaa kuteua mwakilishi mmoja kuhudumu kama kamishna wa tume ya uchaguzi.

Tofauti na pendekezo la kuwa na wawakilishi wa vyama vya kisiasa ambalo lilikubaliwa na mirengo yote, kuna wanaohisi kwamba tume za walimu na maadili na kupambana na ufisadi hazifai kushirikishwa katika tume ya uchaguzi.

Wanaopinga pendekezo hilo wanataka mashirika ya kidini, kupitia miungano yao kuteua mtu mmoja kuwa kamishna wa tume.

Kulingana na mbunge wa Kisumu Magharibi Olago Aluoch ambaye pia ni mwanachama wa JLAC, kamati imepiga hatua kuhusu mabadiliko ambayo inataka yafanyiwe tume huru ya uchaguzi nchini. “Tunaendelea kukutana lakini tumepiga hatua kubwa,” alisema.

Kwenye mswada anaotaka mabadiliko katika IEBC, Bw Kaluma ambaye ni wakili anapendekeza vyama au miungano ya kisiasa iliyo na wabunge wengi na wachache bungeni ipatiwe nafasi tatu katika IEBC na chama cha wanasheria nchini kipatiwe nafasi ya kuteua mwanachama mmoja kuwa kamishna.

Kulingana na mbunge huyo, hakuna mtu nchini asiyekuwa na msimamo wa kisiasa. Kaluma pia ni mwanachama wa JLAC na kulingana na Bi Wahome hajawasilisha mapendekezo yake kwa kamati hiyo.

IPPG ya 1997 ilishirikisha vyama vya Kanu, Democratic Party, Ford Kenya, Ford Asili na Safina ambavyo vilikuwa na vimewakilishwa bungeni. Vyama hivyo vilitengewa nafasi katika iliyokuwa tume ya uchaguzi ya Kenya ECK kwa kutengemea idadi ya wabunge wa kila chama bungeni.

JLAC inatayarishja mabadiliko katika sheria ya IEBC ili kubuni jopo la kuchagua wanaopaswa kuteuliwa kuwa makamishna wa tume hiyo.

Kulingana na Bw Kaluma makamishna wa tume hawafai kutoa eneo moja, dini moja, kabila moja au jinsia moja.