Michezo

Pipeline na Prisons zaanza vizuri voliboli Cairo

March 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KLABU za Pipeline na Prisons kutoka Kenya zimeanza kampeni zao kwenye mashindano ya voliboli ya wanawake ya Afrika vyema jijini Cairo nchini Misri, Jumapili.

Pipeline ya kocha Margaret Indakala imepiga Rwanda Revenue Authority (RRA) kwa seti 3-0 za alama 25-19, 25-19 na 25-15.

Warembo wa Pipeline wanatafuta taji lao la nane la Afrika na la kwanza tangu mwaka 2005. Wako katika Kundi C.

Mechi ya ufunguzi ya kundi hili ilishuhudia FAP kutoka Cameroon ikibwaga Shooting kutoka Misri kwa seti 3-0 za 26-24, 25-14 na 25-22, Jumamosi.

Prisons ilifungua siku kwa kubwaga Asec Mimosa ya Ivory Coast kwa seti 3-0 za alama 25-12, 25-13 na 25-8 katika mechi ya Kundi D.

Vipusa hawa wa kocha Josp Barasa waliibuka malkia wa Afrika mwaka 2008, 2010, 2011, 2012 na 2013.

Walipigwa na GS Petroliers ya Algeria katika fainali ya mwaka 2014. Petroliers wako katika kundi moja na Prisons. Waalgeria hao walinyamazisha El Shams kwa seti 3-2 (25-15, 22-25, 17-25, 25-20, 15-10) Jumamosi.

Wawakilishi wengine wa Kenya, KCB walizaba DGSP kutoka Congo Brazzaville 3-0 (25-14, 25-12 na 25-17), Jumamosi. Wanabenki hawa, ambao ni mabingwa wa Afrika mwaka 2006, hawakushiriki mashindano haya mwaka 2016, 2017 na 2018.

Makundi:

Kundi A: Ahly (Misri), Customs (Nigeria), USFA (Burundi), Canon de Ndjili (DR Congo)

Kundi B: Carthage (Tunisia), DGSP (Congo Brazzaville), KCB (Kenya), Sporting (Misri)

Kundi C: Pipeline (Kenya), Shooting (Misri), Revenue Authority (Rwanda), FAP (Cameroon)

Kundi D: Prisons (Kenya), Asec Mimosa (Ivory Coast), Nkumba (Uganda), GS Petroliers (Algeria), Shams (Misri)