• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Vuta nikuvute kuhusu uongozi wa Joho yafika mbele ya Seneti

Vuta nikuvute kuhusu uongozi wa Joho yafika mbele ya Seneti

Na CHARLES WASONGA

MZOZO katika Bunge la Kaunti ya Mombasa na utawala wa Gavana Hassan Joho Jumatatu ulifika mbele ya Seneti huku gavana huyo akitofautiana na seneta wa kaunti hiyo Mohammed Faki.

Joho ambaye alikuwa amealikwa kutoa maelezo kuhusu uhasama kati yake na bunge la kaunti hiyo alimkashifu seneta huyo kwa kuleta kile ambacho alitaja kama uvumi katika seneti kuhusu mahusiano kati yake na madiwani wa kaunti hiyo.

Huku akiandamana na baadhi ya maafisa wake, gavana Joho alipuuzilia mbali madai kuwa vuguvugu moja linakusanya sahihi kwa lengo la kuvunjilia mbali bunge la kaunti ya Mombasa.

“Sitajibu uvumi na sarakasi za kisiasa ambazo zimeletwa mbele ya kamati hii na seneta wangu. Sijui alizitoa wapi. Juzi niliwaona maseneta wakijadili mizozo katika kaunti ya Mombasa huku wengine wakitumia lugha ya matusi dhidi yangu,” akasema Bw Joho.

Gavana Joho alisema hayo alipokuwa amefika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi inayoongozwa na Seneta wa Laikipia John Kinyua. Aliwataka maseneta hao kutumia muda wao kujadili masuala yenye umuhimu wa kitaifa kama vile baa la njaa, sakata za ufisadi na kudorora kwa uchumi.

“Wakati huu sitajibu chochote kwa sababu hakuna chochote cha kujadili,” Joho akaeleza.

Alikana madai serikali yake inahujumu utendakazi wa madiwani wa kaunti hiyo japo aliungana kuwa kuna “masuala madogo” ambayo yanapasa kutatuliwa.

“Kuna madiwani wachache ambao wanagombana na mawaziri wangu kuhusu usimamizi wa tenda za kuweka taa za barabarani. Na wengine wamekuwa wakimshinikiza Waziri wangu wa Uchukuzi Tawfiq Balala kuwatengea maeneo ya uegeshaji wa magari 200 lakini akakataa” akasema Bw Joho.

“Kwa hivyo, ikiwa baadhi ya madiwani wanataka kumfurusha afisini Waziri huyo kwa sababu hizo basi ningependeka kuwaeleza kuwa nitamtetea waziri wangu kwa jina na ukucha,” gavana huyo akaongeza.

Gavana Joho hata hivyo alisema yu tayari kurejesha hali ya utulivu na ushirikiano kati ya madiwani na maafisa wake kwa ajili ya “kulinda na mafanikio ya ugatuzi”.

You can share this post!

Wakenya watawala Taipei Marathon

Wakurugenzi wa Platinum Distillers washtakiwa kukwepa...

adminleo