• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
KAULI YA MATUNDURA: Mpya kabisa! Kamusi Pevu ya Kiswahili kusambazwa kote nchini na Serikali

KAULI YA MATUNDURA: Mpya kabisa! Kamusi Pevu ya Kiswahili kusambazwa kote nchini na Serikali

Na BITUGI MATUNDURA

MNAMO Juni 6, 2017, mwalimu na rafiki yangu – Prof Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi alinitumia nakala ya kamusi yake – Kamusi Pevu ya Kiswahili (KPK) iliyochapishwa na Vide Muwa Publishers Kenya Limited 2016.

Azma ya kunitumia kamusi hiyo ilikuwa na malengo mawili.

Kwanza, Prof Wamitila alinitaka niifanyie mapitio kwenye magazeti.

Pili, alinitwika jukumu la kuisoma kwa makini na kudokeza mambo madogo madogo yaliyohitaji kuhaririwa kwa nia ya kuiboresha.

Prof Wamitila, ambaye alinifundisha katika Chuo Kikuu cha Nairobi vilevile ni mmoja wa wahakiki na wananadharia wa fasihi na wanaleksikografia wazuri sana Afrika ya Mashariki na Kati – na aliwahi kutuzwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili – TUKI (sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili) kwa mchango wake katika nyanja hizo.

Kila tupatapo fursa ya kuzungumza naye, mimi humtania kwamba yeye ni mmoja wa wasomi ambao aghalabu kazi zake zimerejelewa zaidi katika ukanda huu.

Ni muhali kusoma jarida la kiakademia linalohusu fasihi ya Kiswahili na kukosa kuona kazi yake ikiwa imerejelewa hapa na pale.

Sikuwahi kutimiza azimio la mwalimu wangu kwa sababu ambazo nisingeepuka.

Hata hivyo, juma lililopita, hatua ya Kampuni ya Vide Muwa kuamua kushirikiana na shirika la Uchapishaji la Serikali – Kenya Literature Bureau (KLB) kuisambaza Kamusi Pevu ya Kiswahili imenipa idhini na sababu ya kuizungumzia kamusi hii katika ukumbi huu.

Mtunzi wa Kamusi Pevu ya Kiswahili amejitahidi katika kuingiza na kutomesha maneno mengi ya Kiswahili ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiachwa nje ya kamusi zilizoko tayari.

Aidha, kamusi hii ina kurasa 48 za picha halisi za matunda na njugu, mboga, vyakula na viungo, wanyama, ndege, wadudu, samaki na viumbe wa majini, miti, na mimea.

Picha

Vilevile ina picha za rangi na sauti kama vile kugutia, kugooka, kutatata na kadhalika, picha za zana za teknolojia na usafiri, mazingira na maumbile, wafanyakazi au shughuli tofauti na zana, vifaa au vyombo mbalimbali.

Imeandikwa kwa lugha sahili inayoweza kueleweka na mzungumzaji na msomaji wa kiwango chochote cha Kiswahili.

Hatua ya mtayarishaji wa kamusi kuwashirikisha na kuwahusisha wataalamu mbalimbali wa Kiswahili kutoka ukanda wa Afrika ya Mashariki katika utafiti wake katika maandalizi ya kamusi hii inaonesha kwamba ubia katika ustawishaji wa leksikoni na leksikolojia ya Kiswahili ni mkabala unaoweza kuzaa matunda yenye manufaa sana katika kusukuma mbele kimakusudi maendeleo ya Kiswahili.

Baadhi ya wataalamu walioshirikishwa katika utafiti wa data ya kuandaa kamusi hii ni pamoja na Prof Mohamed Hassan Abdulaziz, Prof Gudrun Miehe, Prof Mugyabuso Mulokozi, Prof James Salehe Mdee, Ustadh Wallah bin Wallah, Prof Kineene Wa Mutiso, Nuhu Zuberi Bakari miongoni mwa wataalamu wengine.

Upanuzi wa mawanda ya usambazaji wa Kamusi hii utachangia kuhakikisha kuwa inawafaidi wapenzi wote wa Kiswahili.

 

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Prof Chimera hana mfano kwa kujitoa...

Kigogo: Tamthilia inayotabiri kuporomoka kwa viongozi...

adminleo