• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
VITUKO: Baada ya dhifa ya Sindwele, Pengo afumaniwa na mke, aishi kama panya

VITUKO: Baada ya dhifa ya Sindwele, Pengo afumaniwa na mke, aishi kama panya

Na SAMUEL SHIUNDU

FURAHA ya Sindwele ilikuwa ya kupigiwa mfano chambilecho waambaji.

Alihitaji sherehe. Alijua kuwa angeshinda kesi yake, lakini hakujua kuwa ingekuwa rahisi ilivyotokea.

Alimtaka Pengo pale Jamhuri kwa sherehe.

Pengo hakuwa radhi kukutana na mwenzake Jamhuri hasa akikumbuka walivyozolewa na askari wiki chache zilizopita.

Alijimithilisha na mtu aliyeumwa na nyoka na kuuogopa ung’ong’o.

“Bwana katafute mahali pengine. Jamhuri pana nuksi!” Wakaafikiana kukutana Sidindi katika mkahawa wa Violin.

Wawili hawa hawakukawia hapo Violin kwani Pengo alikuwa na vifurushi vya karatasi za kusahihishwa.

“Wajua mitihani ya kufunga muhula imeng’oa nanga aisee!” alimkumbusha rafiki yake.

Sindwele hakuhitaji kukumbushwa, naye alikuwa na yake yaliyomharakisha.

Alihitaji kurejea Maka mapema ili asije akakifufua kizaazaa cha kukosa shule tena. Wakaharakisha na kufumkana.

Vituko. Mchoro/ Samuel Muigai

Pengo alipofika nyumbani kwake katika mtaa wa Sidindi, alimpata mgeni ambaye hakumtarajia. Mkewe alikuwa katua mjini kumwona.

Alikuwa kasimuliwa visa vya wanaume wanaotowekea mijini na kuhunika wasizikumbuke tena familia zao kule kijijini.

Aliyoyapata Feliz yalitosha kumhakikishia kuwa Pengo wake alikuwa katika hatari ya kutunduka.

Chumba alichoishi kilikuwa na uholela wa kikapera. Akamwanza na hili.

“Hivi mume wangu waishi kama panya? Tazama nguo chafu zilivyotapakaa ovyo kila mahali! Utanitia aibu mwenzako” alilalamika.

“Wanawake hamwishi vituko. Nikikinadhifisha chumba hiki utanitaka nikueleze anayekinadhifisha, nisipokinadhifisha taabu!” Pengo alimrejeshea mwenzake malalamiko.

Felistus akaufyata. Kwa hakika, aliona heri kuwa na mume mchafu kuliko mume wa kikoa. Akampongeza Pengo wake kimoyomoyo. Akabadili mkondo wa mazungumzo kwa kumuuliza, “Lakini hizi ni saa ngapi unarejea nyumbani mume wangu? Hivi hujui mji huu ulivyo wewe?”

“Nilikuwa nimeenda Violin kukutana na Bwana Sindwele,” Pengo alimjibu.

Feliz hakupenda kusikia kuwa urafiki kati ya mumewe na Sindwele ulikuwa unaendelea.

Mara kadhaa alikuwa kamwonya aepukane na walimu wa shule uchwara kama Maka.

Na huyo Sindwele hakumpenda kabisa! Kwanza mwenyewe kakimbiwa na mke. Halafu uongeze ule ulevi wake. ‘Ni kipi kiwawekacho pamoja?’ alishangaa. ‘Na hilo jina Violin mbona linakaa la kike?’ Akajiuliza.

Sindwele yuyu huyu ndiye aliyewashawishi wazazi wa Pengo wamkubali.

Aliukumbuka msemo alioutumia Sindwele wazazi wa Pengo walipochelea mwanamke kutoka Maka.

Sindwele aliwajibu, ‘Mbuzi hula majani yaliyo karibu na alipofungwa’.

Msemo huu ulikuwa mzuri siku hiyo kwa sababu Pengo alikuwa ‘kafungwa’ Maka na majani yaliyokuwa karibu ni Felistus. Lakini sasa Pengo kahamia Sidindi palipokuwa na majani mengine. Akaamua kusalia pale Sidindi na Pengo wake.

You can share this post!

USWAHILINI: Kujisitiri mwanamke wa Uswahili kiini si dini,...

SEKTA YA ELIMU: Mpango wa elimu ya upili kwa wote...

adminleo